Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala amekataza michango ya aina yeyote itakayosababisha wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2023 washindwe kuripoti shuleni.
Ambapo jumla ya wanafunzi 12,507 Wilaya ya Ilemela waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka mpya wa masomo wa 2023 ambao walipaswa kuripoti shuleni walikopangiwa tangu shule zilipofunguliwa Januari 9 mwaka huu.
Kati ya hao mpaka sasa jumla ya wanafunzi 6367 pekee ndio waliokwisha ripoti shuleni sawa na asilimia 53 ya wanafunzi wote huku wanafunzi 6140 wakiwa hawajaripoti.
Massala ametoa agizo hilo jana wakati wa ziara yake kwa shule za msingi na sekondari zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela yenye lengo la kufuatilia mahudhurio ya kidato cha kwanza, awali na darasa la kwanza.
Pamoja na kusikiliza changamoto za walimu na kuhamasisha ufaulu ambapo amewataka Wakuu wa shule, Maofisa Elimu na viongozi wa mitaa na kata kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanaripoti shuleni na hakuna kuzuia mtoto yeyote kuingia darasani.
“Kuna wazazi mnawazuia eti sababu hawajajaza fomu za kujiunga na shule kwenye kile kipengele cha daktari, wengine kwa kukosa sare, wengine sijui hawana jembe,nasema marufuku kuzuia watoto kwasababu ya michango yeyote,”ameeleza Massala.
Mbali na hayo pia ametaka hatua zichukuliwe kwa wazazi watakaoshindwa kupeleka watoto shuleni pamoja na watendaji watakaokwamisha zoezi la wanafunzi kuripoti shuleni.
Diwani wa Kata ya Mecco Godlisten Kisanga amewaasa viongozi wa mitaa kushirikiana ili kuhakikisha watoto wote wanaripoti shuleni.Huku akiahidi ufuatiliaji wa nyumba kwa nyumba ili kubaini watoto waliochaguliwa na hawajaripoti shuleni.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mwl.Alex Mkusa amewapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha Halmashauri hiyo inaendelea kushika nafasi nzuri kitaifa huku akiwataka kuongeza juhudi katika ufundishaji ili ufaulu kwa nafasi na daraja la ufaulu viende sambamba (GPA).
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini