December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 48 ya wanafunzi hawajaripoti shule

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Rukwa

MKUU wa wilaya Nkasi mkoani Rukwa Peter Lijualikali amewaagiza maafisa watendaji wa kata na maafisa elimu kata kuhakikisha Wanafunzi wote ambao hawajaripoti shule wanakwenda shule kinyume cha hapo wao watonekana kuwa ni wazembe na watawajibishwa.

Akizungumza kwenye kikao cha ushauri cha wilaya (DCC) amesema kuwa katika mkoa Rukwa wilaya Nkasi inaonyesha kuwa ni ya mwisho kwa Watoto kuripoti shule ambapo mpaka sasa asilimia 48 ya Watoto wote wanaotakiwa kuripoti shule hawajaenda shule.

Hivyo ametoa muda hadi jumatano ya wiki ijayo na kama watakua hawajaripoti shule hadi siku hiyo kila mmoja aende na maelezo ya maandishi kueleza ni kwa nini hari ipo hivyo.

Pia ameitaka idara ya elimu kuzitizama shule za Kipili,Wampembe na Kipande ambazo zimefanya vibaya kwenye mitihani yao ya mwaka huu na kuwa haiwezekani shule hizo zikashika nafasi ya mwisho kimkoa huku pia akitaka maelezo ya kina kwa shule ya Kipili kuwa ya mwisho kila mwaka.

Mkuu huyo wa wilaya pia aliitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa shule ya Matala kufanya vizuri na kuongoza kimkoa na kutaka wengine waige kwa shule hiyo.

Katika kikao hicho cha ushauri cha wilaya yalielezwa mafanikio muhimu yaliyotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2022/2023 kuwa ni usajili wa vikundi 67 katika mfumo wa TPLMIS na vikundi 55 katika mfumo wa CMG.

Kufanya ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo ya vikundi vya Wanawake,Vijana na Watu wenye ulemavu ambapo jumla ya Tsh 79,824,000 zimerjeshwa

pia waliweza kulisimia zoezi la sensa kwa kiwango kikubwa kwa asilimia 115 ,kuajiri Watumishi wapya 263 na kupandisha vyeo watumishi 585,Kupandisha uzalishaji wa mazao ya chakula hadi kuwa na ziada ya kutosha.

na wameweza kuongeza usajili wa shule mpya 3 za Sekondari,kusimamia mitihani yote ya kitaifa,kuhamasisha zoezi la upandaji wa miti,kufanya malipo kwa kaya ambazo ni wanufaika wa TASAF ikiwa ni pamoja na hamasa kubwa kwa jamii ya kuwataka kujiunga na mfuko wa bima ya afya ya jamii.
Mwisho