Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia na linaendelea kumhoji John Isaya(21), dereva bajaji na mkazi wa mtaa wa Bukala,Wilaya ya Sengerema mkoani hapa, kwa tuhuma za kutengeneza na kusambaza picha mjongeo kwenye mitandao ya kijamii (Tik Tok) akitangaza kuwa anauza mtoto wake aliyekuwa amembeba kwa mbeleko kwa shilingi milioni 1.6.
Ambapo imeelezwa kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria na ni ukatili kwa mtoto huyo,huku ukamataji wa mtuhumiwa huyo umetokana na taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi makao makuu Dodoma,ambapo ilieleza pia mtu huyo atafutwe, akamatwe ili awaze kuwajibika kisheria kwa kitendo alicho kifanya.
Akizungumza na waandishi wa habari, Januari 6,2025,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, amesema,baada ya taarifa hiyo Januari 04,2025 majira ya saa 2 asubuhi (08:00 hrs), Wilaya ya Sengerema Mkoa wa Mwanza walifanikiwa kumkamata John Isaya, huku chanzo cha tukio hilo ni kutafuta umaarufu kupitia mitandao ya kijamii (Publicity).
Hata hivyo amesema,jeshi hilo linawakumbusha wananchi kuendelea kufichua vitendo vya kihalifu na linawataka waendelee kuvilaani na kuvikemea vitendo vya ukatili wa aina zote, kwani kitendo cha aina hii kama alivyofanya mtuhumiwa huyo kinaweza kusababisha madhara kwa watoto pamoja na kudhalilisha na kushusha thamani ya utu wa mtoto.
More Stories
Kamati ya Mfuko wa Jimbo Musoma Vijijini yagawa vifaa vya ujenzi
Hatma mrithi wa Kinana kupatikana
Mrithi wa Kinana CCM kujulikana katika Mkutano Mkuu wa Jan 18/19