December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asasi za Kiraia zatakiwa kushirikiana na Serikali kuchochea maendeleo ya nchi

Na  Josephine Majura WFM, Dar es Salaam

Serikali imetoa wito kwa Asasi za Kiraia nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika maeneo mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya pamoja kwa kuwa nchi inahitaji mawazo ya pamoja ili kusukuma gurudumu la maendeleo kwa manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb), wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Kitakwimu la Mwaka 2021 (data tamasha 2021) kuhusu matumizi ya takwimu kwenye uchumi wa kidijitali lililofanyika jijini Dar es salaam.

“Nimefurahi kusikia kuwa Asasi hii ya dLab mnafanya kazi kwa karibu na Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na ile ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (OCGS)”alisema Mhandisi Masauni.

“Nimeelezwa kuwa mwaka 2019 wakati Tanzania inaripoti kuhusu utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo ya Mwaka 2030, Asasi ya dLab ilitoa ushirikiano mkubwa kwa Serikali kwenye majadiliano yaliyofanyika jijini New York, Marekani katika Kundi la Asasi za Kiraia”, alisisitiza Mhandisi Masauni.

Alieleza kuwa Jumuiya ya Afrika (AU), kupitia Kikao cha Mawaziri wa Fedha, Mipango na Uchumi kwa pamoja ziliridhia Azimio la “African Data Consensus on Data Revolution” lengo likiwa ni kwa Ofisi za Takwimu katika Bara la Afrika kufanya mapinduzi katika eneo la uzalishaji wa Takwimu kwa ajili ya Serikali.

Aidha aliongeza kuwa mkutano huo uliridhia kutumia vyanzo mbalimbali kutoka katika sekta binafsi, asasi za kiraia, watafiti, wanazuoni na wengine kwa ajili ya kufuatilia Ajenda ya Afrika Tuitakayo ya Mwaka 2063 “Africa we Want”.

Mhandisi Masauni alisema kuwa, Serikali katika kutekeleza azimo hilo imekuwa ikihusisha wadau wote katika mfumo wa kuzalisha na kusambaza takwimu hapa nchini (National Statististical System) ambayo imeelezwa vizuri katika Sheria ya Takwimu SURA 351.

Aliitaka Asasi ya dLab pamoja na Asasi nyingine nchini kuhakikisha zinaendelea  kufuata miongozo mbalimbali katika kuzalisha takwimu zinazofuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Umoja wa Mataifa pamoja na Serikali za Nchi husika iliyowekwa ili kuondokana na upotoshaji wakati wa uandaaji wa takwimu.

Alipongeza dLab kwa kushirikiana na Serikali husasan kwa ufadhili walioutoa wa wanafunzi wa nne kusomeshwa nchini ngazi ya Shahada ya Uzamili kwenye Sayansi ya Takwimu” katika Chuo cha Dar es Salaam.

Mhandisi Masauni aliongeza  kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22-2024/25) wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu ambao umelenga kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati kwa kutumia teknolojia, ubunifu na Sayansi katika sekta za kiuchumi  hususan katika sekta ya fedha kwa lengo la kukuza uchumi na kufikia asilimia 8 hadi 10.

“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha kuwa mada mtakazozitoa kwa washiriki wa Tamasha hili waliopo hapa ukumbini na wale wanaofuatilia kwa njia ya mtandao zilenge kutusaidia namna gani tunaweza kutumia fursa za teknolojia zilizoko katika kuimarisha uchumi wa Tanzania na hususan kipindi hiki ambacho dunia inapambana na janga la ugonjwa wa UVIKO 19”, alisema Mhandisi Masauni”.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. John Sausi, alisema kuwa Serikali chini ya wizara mwaka 2017 ilianzisha Mpango Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya dLab, Bw. Sosthenes Sambua alisema wataendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha malengo ya Taifa yanafikiwa kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa dLab, Steven Chacha, aliwashukuru wadau mbalimbali kwa ushirikiano waliouonesha na  kufanikisha kufanyika kwa Tamasha hilo.

Tamasha hilo la siku tatu linafanyika kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Kitivo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Kampasi ya Kijitonyama, jijini Dar es salaam.