Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Emmanuel Mabura(33), mkazi wa mtaa wa Mhandu kisiwani wilayani Nyamagana mkoani Mwanza,anasakwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Mussa Said(34) mkazi mtaa wa Maswa Magharibi,Kata ya Mhandu,wilayani humo.
Inadaiwa kuwa Mussa ambaye sasa ni marehemu aliyeuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni baada ya kuzuka ugomvi baina yake na mtuhumiwa.
Akizungumzia tukio hilo Oktoba 21,2025,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbord Mutafungwa,amesema Oktoba 19, mwaka huu majira ya saa 1 kamili jioni huko mtaa wa Mhandu Kisiwani,Kata ya Mhandu, wilaya ya Nyamagana, Mussa Juma Said, alifariki dunia baada ya kuchomwa na kipande cha chupa chenye ncha kali na mtuhumiwa Emmanuel Mabura.
Mutafungwa amesema,tukio hilo lilitokea baada ya kuibuka mzozo uliotokana na ushabiki wa mpira wa miguu uliyohusisha timu ya Simba na Yanga, ndipo mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo baada ya kuzidiwa hoja.
Amesema,chanzo cha tukio hilo ni mzozo uliotokana na ushabiki wa mpira ambapo mwili wa marehemu Mussa umefanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na kukabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi.
Sanjari na hayo ametoa wito kwa wananchi kushirikiana kwa kutoa taarifa sahihi zitakazo saidia kumkamata mtuhumiwa aliyehusika na mauaji kisha kutoroka.
“Ninawakumbusha wananchi kuwa na ushabiki wa staha na hakuna sababu ya kugombana au kushambuliana kutokana na tofauti za itikadi za ushabiki wa kitu chochot.Kwani jeshi la polisi halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kufanya uhalifu huo,”amesema Mutafungwa.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako