Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Nzega
WAKALA wa Mbegu nchini (ASA) wanatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mbegu kutoka tani 200 za sasa hadi tani 3000 mwakani.
Hayo yamebainishwa na Mwenyetikiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile mara baada ya kutembelea mradi huo unaotekelezwa na serikali katika
eneo hilo na kupata taarifa ya mafanikio makubwa ya mradi huo.
Alisema kuwa Shamba la Kuzalisha Mbegu la Kilimi lililopo Wilayani Nzega Mkoani hapa lina uwezo mkubwa sana wa kuongeza uzalishaji wa mbegu kama litawezeshwa ili kuboresha shughuli zake ikiwemo kutumia Teknolojia ya Umwagiliaji ambayo itachochea uzalishaji wa mazao ya wakulima.
Alibainisha kuwa kuboreshwa kwa teknolojia ya umwagiliaji kutaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii hapa nchini kupitia sekta ya kilimo.
Mariam alishauri serikali kuendelea kuwekeza miradi hiyo katika maeneo mengine nchini ili kurahisisha upatikanaji wa mbegu bora kwa bei ya chini.
Aliitaka Wizara ya Kilimo kuwezesha Wakala huo ili kuboresha zaidi shughuli zao ikiwemo teknolojia ya umwagiliaji.
Kamati hiyo ilipongeza kazi nzuri inayofanywa na Wakala wa Mbegu nchini (ASA) ila ikawataka kutumia ipasavyo fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya mradi huo. Â
Mwenyekiti alifafanua kuwa kupitia teknolojia ya umwagiliaji uzalishaji wa mbegu utaongezeka kutoka tani 200 kwa mwaka 2022 hadi kufikia tani 3000 kwa mwaka 2024 hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya mbegu nchini .
Awali Naibu Waziri wa Kilimo Davidi Silinde aliiambia Kamati hiyo kuwa serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuboreshwa shughuli za Wakala wa Mbegu nchini ili kuwawezesha kuzalisha mbegu kwa kipindi chote cha mwaka .
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha nchi inazalisha mbegu nyingi ili kuwezesha wakulima kuzipata kwa wakati badala ya kuendelea kuagiza mbegu hizo kutoka nje ya nchi na kutumia fedha nyingine za kigeni.
Hata hivyo alisisitiza kuwa kazi ya kuzalisha mbegu sio ya serikali pekee, hivyo akaomba sekta binafsi kuisaidia serikali kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mbegu.
Naibu Waziri aliwatoa hofu wazalishaji wa mbegu na kuwahakikisha kuwa serikali itawaunga mkono ikiwemo kuwapatia elimu ya uzalishaji mbegu bora.
Shamba la mbegu la Kilimi huzalisha mbegu za alizeti, choroko ,mahindi na mtama na kuzisambaza kwa wakulima katika Kanda ya Magharibi na Ziwa.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa