November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Apandishwa kizimbani kwa tuhuma za kufanya mapenzi na mtoto wake

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira online, Mwanza

Mkazi wa Nyakato mkoani Mwanza, Bashiri Mohamed (35), amefikishwa mahakamani Mei 21,2024 na kusomewa shtaka moja la kuzini na maharimu.

Mshtakiwa huyo amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza na kusomewa shtaka hilo kosa analodaiwa kulitenda kati ya Septemba,2023 hadi Februari 15, 2024.

Akisoma shtaka hilo,Mwendesha Mashtaka wa Serikali Mwanahawa Changale amesema; “Mshtakiwa kwa tarehe tofauti kuanzia Septemba 2023 hadi Februari 15, 2024, eneo la Nyakato-Mecco, wilayani ya Ilemela anadaiwa kuzini na maharimu (16) huku akitambua ni mtoto wake wa kumzaa.”

Amesema mshtakiwa ametenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 158 (1) (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

Hata hivyo, baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa amekana shtaka na kuomba apatiwe dhamana.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, wa mahakama hiyo Juma Opudo amemtaka mshtakiwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili watakosaini hundi ya maneno ya milioni 4 kila mmoja na mwingine awe na mali isiyohamishika.

Hata hivyo, mshtakiwa amekwama kutimiza masharti ya dhamana kwani barua ya udhamini ya mdhamini mmoja aliyetokea wilayani Magu haikuthibitishwa na Hakimu Mfawishi wa Wilaya yake.

“Barua yako sitoipitisha kwa sababu unatokea Wilaya nyingine na haijapita kwa Hakimu Mfawidhi wa Wilaya unayotoka. Shauri litaitwa kesho kwa ajili ya kutajwa ili kukamilisha mchakato wa dhamana,” amesema.

Hakimu ameahirisha Shauri hilo hadi Juni 11, mwaka huu litakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kusomewa hoja za awali.