November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ana ahidi,ana tekeleza,maneno kidogo,vitendo vingi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Morogoro

Katika ziara yake ya kihistoria mkoani Morogoro Agosti 4,2024, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amedhihirisha tena dhamira yake ya kuleta maendeleo endelevu na kuinua maisha ya wananchi.

Rais amefanya shughuli kadhaa muhimu, ambazo zimeleta matumaini makubwa kwa wakazi wa Morogoro na taifa kwa ujumla.

Kwanza, Rais Samia ameweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa majengo ya kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Hii ni hatua kubwa katika sekta ya elimu, inayolenga kuongeza nafasi za masomo na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Kwa kujenga kampasi hii mpya, serikali inaonesha kuwa ina nia thabiti ya kuwekeza katika elimu na kuandaa wataalamu mahiri kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.

Rais Samia ndio kiongozi pekee wa chama cha siasa ambae ameweka elimu kama kipaumbele.

Ni lini mara ya mwisho kusikia viongozi wa upinzani wakizungumzia suala la elimu?,elimu ilimuinua Rais Samia nae anataka elimu iwainue mamilioni ya Watanzania wengine.

Pia, Mhe. Rais amesalimia wananchi katika round about ya Mikumi, akionyesha ukaribu wake na wananchi wa kawaida. Huu ni uthibitisho wa jinsi Mhe. Rais anavyojali na kuthamini mawazo na hisia za wananchi wake, akijenga mazingira ya uwazi na ushirikiano.

Maelfu ya wananchi walifurika kumuona Rais wa kwanza mwanamke,uwepo wake umewapa matumaini maelfu ya wakazi wa Morogoro kuwa inawezekana.

Katika hatua nyingine muhimu, Rais Samia ameweka jiwe la msingi ujenzi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero (K4) na kuzungumza na wananchi.

Kiwanda hiki kipya kitaleta ajira nyingi kwa wakazi wa eneo hilo na kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, jambo ambalo litapunguza utegemezi wa uagizaji wa sukari kutoka nje.

Anaposema ajira ni kipaumbele cha awamu yake si tu maneno bali anaonesha kwa vitendo.

Ikumbukwe wakati anaapisha Mawaziri wapya alimuagiza Waziri mpya wa Vijana, Kazi na Ajira kuandaa ripoti ya ajira ngapi mpya zitakua zimeanzishwa ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Kwa bahati mbaya viongozi wa upinzani ajira pekee wanazojali ni za kwao na ndio maana kuna viongozi wa vyama vya siasa ambao wako madarakani tangu enzi za awamu ya tatu mpaka leo.

Aidha,ametembelea na kukagua kituo cha kupoza umeme cha Ifakara, akihakikisha kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika unakuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku ya wananchi wa Morogoro na maeneo mengine ya nchi.

Upatikanaji wa umeme ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya viwanda, biashara na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Rais Samia aliahidi kufanya tatizo la umeme kuwa la kihistoria. Wengi waliahidi hivyo huko nyuma ila ni yeye pekee anayeelekea kutumiza hiyo ahadi.

Kwa ujumla, ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Morogoro imeleta mwanga mpya wa matumaini na maendeleo kwa wananchi wa Mkoa yhuo na nchi kwa ujumla.

Sasa hivi kila eneo la Tanzania wanatamani wapate bahati ya ziara ya Rais Samia. Kila sehemu wanaimba “Mlete Samia! Mlete Samia!” Anaahidi, anatekeleza, kazi iendelee!