March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Allspice’ yatua rasmi Tanzania ,TARI yafungua milango ya kilimo kipya mti wenye harufu ya kiungo zaidi ya kimoja

Na Joyce Kasiki Timesmajira online

Wananchi wanaotembelea Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, wamevutiwa na kiungo kipya cha chakula kijulikanacho kama ‘Allspice’, kilicholetwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

Kiungo hicho ambacho kinapatikana kupitia mti wa asili ya Karibiani, kimewasilishwa kwa mara ya kwanza kwa umma wa Tanzania kupitia Banda la TARI, ambapo wananchi wamepata fursa ya kunusa na kujifunza matumizi mbalimbali ya mmea huo wa kipekee.

Akizungumza Julai 3 ,2025 na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya Kimataifa ya 49 ya Biashara jijini Dar es Salaam , Mtafiti kutoka TARI Kituo cha Mlingano Tanga, Dkt. Mgaya Maumba, alisema Allspice ni kiungo chenye ladha na harufu inayofanana na mchanganyiko wa karafuu, mdalasini, iriki na viungo vingine, na kwamba kina manufaa lukuki kwa afya ya binadamu.

“Mti huu unaojulikana kama Allspice au mchanganyiko wa viungo, una harufu ya aina yake ambayo haipatikani kwa mti mwingine mmoja. Wataalamu wanasema una uwezo wa kusaidia mmeng’enyo wa chakula, kupunguza maumivu ya misuli, kichwa na meno, pamoja na kushusha presha ya damu,” alisema Dkt. Maumba.

Aliongeza kuwa kiungo hicho kimekuwa sehemu ya tiba mbadala katika nchi kama Jamaica na Marekani, ambapo hutumika kutibu maumivu ya hedhi kwa wanawake, kuimarisha kinga ya mwili, na hata kusaidia kupambana na saratani ya matiti na tezi dume.

Katika banda la TARI, wananchi walipata nafasi ya kujionea miche ya mti huo pamoja na maelekezo ya namna ya kuupanda, kuutunza, na kutumia sehemu mbalimbali kama majani, matunda na magome.

“Tunashauri wananchi watumie zaidi majani badala ya magome ili kulinda uhai wa mti na kwamba Allspice inaweza kutumika kama kiungo cha chai, mapishi ya biriani, mikate ya kuokwa na hata bidhaa kama ice cream,” aliongeza Dkt. Maumba.

TARI imehimiza wakulima na wawekezaji kujitokeza kuchangamkia fursa ya kulima mmea huo ambao una soko la kimataifa na unaweza kuwa chanzo kipya cha kipato vijijini ikiwa utapewa kipaumbele kwenye sera za kilimo na utafiti.