January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aliyetuhumiwa kumteka Mo Dewji aachiwa

Grace Gurisha, TimesMajira Online

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imemuachia huru dereva taksi, Mousa Twaleb aliyekuwa akituhumiwa kuhusika kwenye utekaji wa Mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’.

Maamuzi hayo yametolewa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwasilisha mahakamani hapo hati ya nia ya kutokuendelea kumshtaki.

Akizungumza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wa Mahakama hiyo, Wakili wa Serikali, Ester Martin amedai kesi hiyo imekuja kwa kutajwa na pia DPP amewasilisha hati ya kutokuwa nia ya kutokuendelea na mashtaka dhidi yake.

Baada ya Martin, kueleza hayo, Hakimu Shaidi alimueleza mshtakiwa kuwa ameachiwa huru na aondoke ndani ya chumba cha mahakama.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo baada ya kuachiwa aliwekwa tena chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi, ambapo aliondoka mahakamani akiwa na askari kwa kuelekea kituo cha Polisi.

Itakumbukwa kuwa, June 16,2021 Wakili wa Serikali, Faraja Ngukah aliieleza Mahakama hiyo kuwa, DPP baada ya kupokea malalamiko ya mshtakiwa huyo atatoa maelekezo kuhusu jalada hilo kutokana na upelelezi kutokukamilika.

Pia kabla ya maamuzi ya kumuachia huru Twaleb, Ngukah aliomba shauri hilo lipangiwe muda mfupi ili kusubiria maelekezo ya DPP, kwa sababu tayari majalada mengine ameshaanza kuyafanyia kazi kwa muda mfupi.

Kwa upande wa Wakili wa Utetezi, Richard Rweyengeza amedai, hata yeye alikutana na DPP amemuhakikishia kwamba majalada yaliyoitwa ni pamoja na jalada la mteja wake na pia DPP alimueleza kuwa alipokwenda gerezani Twaleb alimlalamikia sana.

Baada ya mawakili hao kudai hayo, Hakimu Shaidi amesema hata DPP alivyokuja kutembelea Mahakamani hapo alimueleza kuhusu kesi hiyo, kwa hiyo mshtakiwa awe na subira malalamiko yake yanafanyiwa kazi.

Awali,  Wakili wa mshtakiwa huyo, Mahfudhu Mbagwa amedai kuwa Machi 24,2021 upande wa mashtaka ulidai wamemkamata mshtakiwa mwingine Afrika ya Kusini, wanafanya utaribu wa kumleta Tanzania.

Mbwaga amedai, kwa hatua iliyofikia sasa, hatua zingine zinatakiwa kuendelea kwa mshtakiwa ambae yuko mahakamani, kwa sababu hakuna kinachoendelea hivi sasa.

Akijibu hoja hizo, Ngukah amedai, shauri hilo ni la uhujumu uchumi na wakili Mbagwa anataka Mahakama itoe amri kwenye kesi hiyo, kwenye kesi ya uhujumu uchumi ni hadi DPP atoe kibali cha kusikilizwa na ni baada ya upelelezi kukamilika.

“Hii kesi ni moja ya kesi ya muda mrefu  ambazo tumezifikisha mbele ya DPP kwa sababu yeye ndiyo mwenye kushtaki na kufuta,” amedai Ngukah

Akijibu hoja ya mshtakiwa aliyekamatwa Afrika Kusini, Ngukah amedai ni kweli alichokidai wakili kuwa kuna mshtakiwa alikamatwa na wapo kwenye utaratibu wa kumleta Tanzania.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Shaidi amesema, kutokana na kesi hiyo kuwa ya muda mrefu na aiendelei mbele, katika kikao ambacho wamekifanya hivi karibuni kilichoudhuliwa na wawakilishi wa DPP aliipendekeza hiyo kesi kwa ajili ya hatua zaidi.

“Kwenye kesi yako niliitolea mfano ni kesi ambayo sijaridhika nayo, kama wewe unakosa lako basi liendelee na wale washtakiwa wengine wakikamtwa basi na wao washtakiwa sio wewe una kaa tu gerezani ukisubiri wao wakamatwe,” amesema Hakimu Shahidi

Hakimu huyo, alikwenda mbali zaidi kuwa, kama imeshindikana kwa mshtakiwa kushtakiwa kwa kosa lake, basi aachiwe kwa kupewa dhamana ya Polisi wakati anasubiri wengine wakamatwe.

Baada ya hakimu kusema hayo, Twaleb alinyoosha mkono na kumueleza hakimu kuwa hajamteka Mo na wala, Mo mwenyewe hamfahamu, kwa hiyo hajui kinachoendelea kwake.

Watuhumiwa wengine ambao upande wa mashitaka inawatafuta ni raia wanne wa Msumbiji na mmoja wa Afrika Kusini wanaodaiwa kumteka mfanyabiashara huyo.

Washitakiwa hao ambao ni Phila Tshabalala raia wa Afrika Kusini, Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji.

Katika kesi hiyo inadaiwa Mei Mosi na Oktoba 10, 2018, katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg Afrika Kusini, kwa makusudi washitakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu.

Pia, inadaiwa Oktoba 11, mwaka jana maeneo Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara MO kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Inadaiwa Julai 10, mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha ambazo ni Sh 8,000,000 wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

MO alitekwa nyara Oktoba 11, mwaka jana alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika eneo la Gymkhana.