Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Tanga
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Tanga,Rashid Hamza, amehama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM),akieleza kuwa sababu kubwa ya uamuzi wake ni kuridhishwa na utekelezaji wa maendeleo aliyokuwa akiidai kwa muda mrefu.
Ambapo amesisitiza kuwa miradi mingi aliyokuwa akiipigania kwa miaka 30 sasa imetekelezwa chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Hamza ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa CUF, baadaye akajiunga na ACT-Wazalendo kabla ya kuhamia CHADEMA.Katika kipindi chote hicho amekuwa mmoja wa viongozi wa upinzani waliokuwa wakijulikana kwa msimamo mkali dhidi ya CCM.
Hamza amepokelewa rasmi Leo Julai 6, 2026, katika Ofisi za CCM Mkoa wa Tanga na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa pamoja na wanachama wa chama hicho.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Tanga mara baada ya kupokelewa,Hamza amesema baada ya takribani miaka 30 ya kufanya siasa za upinzani, hana tena hoja za kuendelea kuikosoa Serikali.
“Nimekuwa nikifanya siasa kwa muda wa miaka mingi takribani miaka 30.Kila kitu nilichokuwa nakipigia kelele pamoja na wenzangu kimefanyika.Bandari ya Tanga imejengwa,barabara nyingi zimejengwa.Hivyo leo najiunga na CCM kwa sababu sioni sababu ya kuendelea kuwa upande wa upinzani,”amesema Hamza.
Pia amesisitiza kuwa amefanya uamuzi huo kwa hiari yake mwenyewe bila kushawishiwa na mtu yeyote.
“Nimejiunga na CCM kwa ridhaa yangu mwenyewe na nikiwa na akili timamu. Taarifa kwamba nimelipwa fedha ili nihame chama si za kweli,”amesema Hamza.
Hata hivyo amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah, kwa ushirikiano aliouonesha hadi kufanikisha hatua hiyo, huku akimpongeza kwa juhudi za kuimarisha chama mkoani humo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah, amesema Hamza ni mwanasiasa aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za upinzani mkoani humo, na kwamba kujiunga kwake na CCM ni nyongeza muhimu kwa chama hicho.
“Mkizungumza kuhusu upinzani Wilaya ya Tanga, baba yake ni Rashid Hamza Jumbe.Wanachama wa CCM ni mashahidi,kila tuliposikia kuna mkutano wa CHADEMA tulijua Rashid anakuja kutupa wakati mgumu,leo ameamua kujiunga na CCM,”amesema Abdallah.
Ameongeza kuwa kuhamia kwa Hamza ni ishara ya kuendelea kudhoofika kwa upinzani ndani ya Mkoa wa Tanga na kwamba atatumika kueleza mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


More Stories
Ndejembi ajadili awamu ya pili ya mradi wa umeme wa jua kishapu
Airtel yaweka alama ruaha Marathon 2026
Viongozi wa vyama vya siasa Mbeya wahimiza amani