Na Esther Macha, Timesmajira Online, Rungwe
MAHAKAMA ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya imemhukumu kifungo cha miaka (2)Msanii wa Sanaa ya uchoraji aitwaye Shedrack Chaula (24) au kulipa faini ya milioni 5 kwa kosa la kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandaoni 2015.
Akisoma hati ya mashtaka leo Julai 4,2024 Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Rosemary Mgeniji mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe Ramla Shehagiro ameeleza kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 22,2024 katika kijiji cha Ntokela wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
Imeelezwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka kuwa mshtakiwa huyo akiwa dukani kwake maeneo ya Ntokela alirekodi ujumbe wa video wenye maneno“Kwakua umeshindwa kutetea taifa lako lisiathirike na ushoga hii video inakuhusu wewe na si mtu mwingine” ikiwa ni taarifa za uongo zenye kupotosha jamii.
Alipopewa nafasi ya kujitetea mahakamani hapo mtuhumiwa huyo Shadrack Chaula mkazi wa Ntokela amesema yupo tayari kutumikia adhabu yoyote atakayopewa na mahakama hiyo.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mawakili wa Serikali Veronica Mtafya na Rosemary Mgeniji umeiomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine kwani kitendo hicho kimetafsiriwa kama udhalilishaji kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe ,Ramla Shehagiro amesema kwa mujibu wa sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 kifungu cha 16 amemtia hatiani kwenda gerezani kutumikia kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya mil.5.
Hata hivyo mtuhumiwa amepelekwa gerezani kwenda kutumikia kifungo baada ya kushindwa kulipa faini.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba