Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
WAISLAMU na wasio waumini wa dini hiyo wametakiwa kuwachukua watoto yatima na kuwalea katika maadili mema,kuwatendea wema na haki ili wasiwakumbuke wazazi wao.
Rai hiyo ilitolewa jijini hapa na Mshauri wa Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Yusuf Swaleh Banyanga, wakati akizungumza baada chakula cha hisani kilichoandaliwa na BAKWATA ikishirikiana na Kampuni ya The Rocky Solutions (T) Ltd kwa ajili ya watoto yatima,masikini na wajane.
“Utaratibu huu wa kuandaa chakula na kula pamoja na watoto yatima,wajane na maskini ni mzuri na isiwe katika hadhara tu, ikiwezekana muislamu hata asiye muislamu akachukua yatima wawili akawalea kwa wema na kuwatendea haki,tukifanya hivyo Mungu atatuepusha mabalaa katika jamii na kwenye shughuli zetu,”amesema Banyanga.
Mshauri huyo wa Sheikh wa Mkoa amesema kuandaa chakula cha yatima, masikini na wajane ili kupata baraka na thawabu, imekuwa ada kwa Sheikh Kabeke katika kuenzi mafundisho ya Mtume Muhhamad S.A.W.
Amesema waislamu hawapaswi kumwachia jambo hilo Sheikh Hassan Kabeke peke yake,kila mmoja ajitoe na kutoa sadaka yake ili Mwenyezi Mungu amlipe kheri,alimpongeza Sheikh huyo wa Mkoa alivyoibadilisha BAKWATA na kukifanya chombo hicho kuaminiwa na waislamu bila kujali itikadi zao za kidini.
Banyanga akizungumzia mmomonyoko wa maadili,amesema janga hilo la kitaifa linasababishwa na wazazi kutokuwa karibu na watoto,hivyo siku ya kiama kila mzazi ataulizwa alichokifanya kwa malezi ya watoto.
“Mzazi ni kiongozi wa familia, ni vizuri kuwapa watoto malezi bora na elimu ya dini kwa sababu chanzo cha mmomonyoko wa maadili kwa vijana ni wazazi kutowalea katika maadili ya dini,wanapaswa kuwapa maadili kuepuka ulawiti,ndoa za jinsia moja na mengine yanayomchukiza Mwenyezi Mungu,”amesema.
Naye Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya The Rocky Solutions (T) Ltd, Diana Magesa,amesema kwa miaka sita kampuni hiyo imekuwa ikiandaa chakula cha pamoja kwa yatima na makundi mengine ikishirikiana na BAKWATA Mkoa wa Mwanza.
“The Rocky Solutions tunafanya haya kurudisha kwa jamii faida tunayopata tukishirikiana na BAKWATA,si Mwanza tu pia tunafanya katika Wilaya ya Kahama (Shinyanga) kwa kusaidia makundi yenye mahitaji wakiwemo yatima na baadhi tunawasomesha,”amesema.
Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii,Wilaya ya Nyamagana,Salum Anatory ameipongeza BAKWATA kwa kuwatambua watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kuwarejeshea tabasamu huku akisema malezi ya watoto ni jukumu la jamii,ni wajibu wa wazazi kuhakikisha wanapata malezi bora na elimu iliyo urithi wa maisha yao ya baadaye.
Awali Sheikh Kabeke amesema tangu alipothibitishwa kushika wadhifa huo mwaka 2019 amekuwaa na desturi ya kufanya shughuli tatu za dini ya kiislamu,akiandaa chakula cha yatima akishirikiana na Mkurugenzi wa The Rocky Solutions,Zakaria Nzuki ingawa si muislamu.
“Zipo nyumba zinalea yatima kwa wema mbinguni hung’aa kama nyota na Malaika huulizana ni nyota gani hiyo,hujibizana si nyota bali nyumba inayohifadhi yatima,lakini zipo nyumba zinawalea yatima na kuwageuza wafanyakazi,Mwenyezi Mungu anatatuka tuwatendee wema,haki na tusiwanyanyase,”amesema.
Sheikh Kabeke ameiomba The Rocky Solutions iendelee kuyatenda hayo kwa wengine kwa maslahi uislamu na kumcha Mungu huku akiwashukuru waandishi wa habari kwa mchango wao wakuielimisha jamii na kuifanya BAKWATA chombo kuheshimiwa na umma.
Kwa mujibu wa Sheikh Kabeke mbali na chakula hicho cha pamoja zaidi ya vituo 17 vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu,wajane na kaya masikini 40 wakiwemo wanafunzi zilinufaika kwa msaada wa kilo 750 za mchele,mafuta ya kula na nyama ya ng’ombe.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba