January 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Alama saba muhimu za Rais Samia kwenye mkutano G20

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

KATI Novemba 18 ha 19, Mwaka huu macho ya dunia yalielekezwa katika Jiji la Rio de Janeiro, nchini Brazil, ambako ulikuwa ukifanyika mkutano wa viongozi wa G20.

Macho ya Dunia yaliangazia mkutano huo, hasa kwa kuzingatia kwamba vingozi hao wa mataifa ya 20 ndiyo wanaotoa mwelekeo wa Dunia, kutokana na mataifa hayo kuwa na uwezo mkubwa kiuchumi.

G20 inaundwa na Argentina, Australia, Brazili, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japan, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Korea Kusini, Uturuki, Uingereza na Marekani.

Kundi hilo linaangalia ukuaji wa uchumi duniani, kushughulikia masuala muhimu ya kimataifa kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, usalama wa nishati na maendeleo, na kukuza ushirikiano wa kimataifa katika masuala muhimu kama vile biashara, fedha na uwekezaji.

Mataifa mengi yalikuwa yakifuatilia mkutano huo ili kujua ni mambo gani yatajadiliwa na kuazimiwa na mataifa hayo makubwa.

Mkutano wa mwaka huu wa G20 umeacha alama kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwake mwenye, Tanzania na Afrika kwa ujuma.

*** Alama ya kwanza kwa Rais Samia mkutano wa G20

Kwenye mkutano huo, Rais Samia, ameacha alama ya kualikwa kushiriki mkutano ambao ulikuwa na kauli mbiu isemayo; “Kujenga Ulimwengu wa Haki na Sayari Endelevu.”

Kualikwa kwa Rais Samia ilikuwa ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kuonesha mchango wake katika masuala ya kimataifa.

*** Alama ya pili

Alama ya pili ambayo ameacha Rais Samia kwa kualikwa kushiriki kwenye mkutano ni kuwa Rais wa kwanza mwanamke kuhudhuria mkutano huu kwa Afrika.

Pia Rais Samia ameacha alama ya kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kushiriki mkutano wa G20 tangu kundi hili linapanuke kutoka G8 hadi G20 mwaka 2009.

Mwaliko wa Rais Samia kushiriki mkutano huo ulitoka kwa Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil.

***Alama ya tatu kupitia mwaliko huo kwa Rais Samia

Alama ambayo imeachwa na Rais Samia kupitia mwaliko kuwa ni ishara ya utambuzi wa juhudi zake kubwa katika kuimarisha utawala bora, kukuza demokrasia na kuleta maendeleo endelevu nchini Tanzania.

Ingawa Tanzania haijawahi kuwa sehemu ya kundi la G20 kabla ya Rais Samia, nchi yetu inayo historia ya kushiriki mikutano ya G8 kupitia Rais Mstaafu Hayati Benjamin Mkapa na Rais mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete, ambao walishiriki mikutano ya G8 mwaka 2005 na 2008.

Hivyo, ushiriki wa Rais Samia katika G20 ni hatua muhimu katika kuendeleza uhusiano wa kimataifa na kuongeza ushawishi wa Tanzania duniani.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unasisitiza nguvu inayokua ya nchi yetu na azma yake ya kuchangia katika kushughulikia changamoto kubwa za kimataifa.

Mfano, Tangu Rais Samia, alipoingia madarakani, ameonesha mwelekeo wa kipekee wa kiutawala, akilenga mageuzi katika sekta mbalimbali.

Juhudi zake za kuhakikisha uwazi katika utendaji wa Serikali, kupambana na rushwa, na kuboresha haki za binadamu – hasa haki za wanawake, vijana, na makundi maalumu, zimeleta mafanikio makubwa.2

Huu ni ushahidi wa mabadiliko ambayo Tanzania imefanya chini ya uongozi wake na ni kipengele muhimu kitakachowezesha nchi kufaidika na jukwaa la G20.

***Alama ya nne

Kwa upande mwingine, mkutano wa G20 umetoa fursa kwa Tanzania kutafuta ushirikiano na ufadhili kwa miradi mbalimbali, hasa katika maeneo ya nishati safi ya kupikia, kilimo kilichozingatia mabadiliko ya tabianchi, na maendeleo endelevu ya kiuchumi.

Katika kipindi cha mabadiliko ya tabianchi, umaskini, na changamoto ya usalama wa chakula, Tanzania ina mchango muhimu wa kimataifa katika kutafuta suluhisho.

Ushiriki wa Rais Samia katika G20 unatoa fursa ya kujenga ushirikiano wa kimkakati na mataifa mengine ili kuhakikisha maendeleo endelevu na kupambana na changamoto zinazokumba dunia kwa ujumla.

Ushiriki wa Rais Samia pia unatoa mfano wa jinsi viongozi wa Afrika, na hasa wanawake, wanavyoweza kuwa na sauti kubwa kwenye masuala ya kimataifa.

Rais Samia amekuwa kielelezo cha uongozi thabiti, na kwa mara nyingine, amethibitisha kuwa Tanzania inajivunia kuwa na Rais ambaye ni kiongozi wa kimataifa.

*** Alama ya tano

Ushiriki wake katika G20 ni ishara kwamba Tanzania ina nafasi muhimu katika kujenga ulimwengu wa haki na sayari endelevu.

Huo ulikuwa ni wakati muhimu kwa Tanzania kwa kujiunga na mataifa mengine ya G20. Kupitia mkutano huo, Tanzania ilipata nafasi ya kuongeza ushawishi wake kwa ajili ya kuleta manufaa kwa wananchi wake, na kujitokeza kama kiongozi wa kimataifa anayeleta mabadiliko chanya.

Rais Samia alionesha uwezo wa kuongoza, na ushiriki wake katika G20 ni uthibitisho wa mafanikio ya kisiasa na kiuchumi yanayoendelea nchini Tanzania.

*** Alama ya sita manufaa ya mkutano huo

Alama ya sita ni manufaa mkutano huo kwa Tanzania . Manufaa hayo yaliakwa na Rais Samia Suluhu Hassan, wakati akizungumza na wahariri vya vyombo vya habari jijini Rio de Janeiro baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

Rais Samia alisema ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano wa G20 una manufaa makubwa kwa Tanzania, lakini pia kama Afrika.

Alisema anashukuru kwa mwaliko, maana Tanzania sio mwanachama wa G20, lakini wameona kuna sababu ya kutuliaka kama Tanzania kushiriki kwenye mkutano huo.

“Kwa sababu kama mnavyojua kundi la G20 ni nchi zote zilizoendelea na zenye uchumi mkubwa, kwa hiyo ukipata fursa ya kualikwa na kupewa nafasi ya kusema, kwanza hayo ni mafanikio, kutambulika, kuitwa na kusema mbele yao,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alisema kwenye mkutano huo walikuwa na mambo matatu makubwa yaliyojadiliwa

***Kuondoa njaa

Rais Samia suala la kwanza walilozungumzia ilikuwa ni kuondoa njaa, ambapo walifanya tathmini ni kwa kiasi gani dunia imeweza kuondoa njaa.

“Tumeona kazi haijafanyika vizuri kwa sababu kuna watu wengi duniani bado wana matatizo ya njaa na sio Afrika peke yake na katika maeneo mengine duniani tofauti.

Kwa hiyo katika kulizungumza hili nchi nyingi zimetoa mikakati ya nini tufanye kupunguza njaa, lakini kuna zile ambazo hali zao ni nzuri wameweza kutoa matumaini na ahadi za kusaidia kifedha, kiufundi, teknolojia na mambo mengine ili kuondosha njaa,” alisema Rais Samia na kuongeza;

“Kwa upande wetu (Tanzania) tulipopewa nafasi ya kusema kwenye hili, tulizungumza hali halisi Tanzania kwamba sisi Tanzania tukienda kama hali ilivyo, bila kuathiriwa na matukio yoyote ya mabadiliko ya tabianchi, basi tunajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128 na tunaweza kuwauzia wenzetu.

Lakini tuna uwezo wa kuzalisha zaidi na tukaweza kulisha majirani, kulisha bara la Afrika na hata nchi za nje ya Afrika.”

Rais Samia alitoa mfano kwa akisema kwa sasa hivi kuna mazao ya mboga mboga ambayo Tanzania inasafirisha mpaka Ulaya, lakini kuna mahindi na mpunga ambayo Tanzania inalisha nchi za jirani.

Kwa upande wa maharage, Rais Samia alisema Tanzania inalisha China. ” Tunalisha China Soya na Soya yetu wanaipenda kweli kweli Wachina, ila tuna vikwazo ambavyo tukisaidiwa tunaweza kuzalisha zaidi,” alisema.

***Ataja vikwazo kwenye kilimo

Rais Samia alitaja kikwezo cha kwanza ni tafiti za kilimo. Katika eneo hilo alisema wanadhani kuna haja ya kuongeza nguvu kwenye tafiti hasa kwenye mambo ya kilimo.

Alitaja eneo la pili kuwa ni masuala ya mambo ya kutumia mashine katika kilimo , matrekta, mashine za kuvunia, mashine za kumwagilia na mambo kama hayo.

“Tukiweza kufanya hivyo tunaweza kuzalisha chakula kingi sana,” alisema.

***Mbolea

Rais Samia alisema tatizo lingine lingine ni mbolea, ambapo kwa muda mrefu Tanzania tunanunua mbolea kutoka nje.

“Ndani nadhani tuna viwanda viwili vya kuzalisha mbolea, lakini pamoja na viwanda hivyo vya ndani, bado tunaagiza mbolea kutoka nje , nadhani kazi yetu ni kuvutia wawekezaji wa viwanda vya mbolea kuja kuwekeza halafu tuweze kuzalisha na kusabamza mbolea ya kutosha kwa wakulima wetu,” alisema Rais Samia na kuongeza;

“Kwa sababu ukiangalia viwango vya matumizi ya mbolea Duniani, Tanzania hatujafika hata nusu kwa heka, kwa hiyo tukiweza kutumia mbolea vya kutosha, mbolea zinazotakiwa, kwa mfano Intercom pale wanazalisha mbolea ambayo wanachanganya na mbolea kidogo ya viwandani na mambo mengi ni yale yale yanayopatikana ndani ya nchi, wanachanganya wanazalisha na mbolea inakuwa nzuri,” alisema.

Rais Samia alisema kwenye mambo hayo matatu tukiweza kufanya vizuri Tanzania kweli inaweza kulisha bara la Afrika, lakini na dunia pia.

“Kwa sababu kama mbogamboga zetu na maharage yanakwenda Ulaya na mambo mengine, asali maeneo mengine duniani huko ni kulisha Ulimwengu.

Kwa hiyo tukiongeza jitihada hayo mambo hayo matatu niliyoyasema tutaenda kufanya vizuri.”

***Jambo la Pili kwenye mkutano wa G20

Rais Samia alitaja jambo la pili ambalo walizungumza kwenye mkutano huo ni safari kutoka hapa tulipo kwenye matumizi ya diseli kwenda kwenye matumizi ya nishati jadidifu (nishati inayotokana na maji, jua na upepe.

Alisema wenzetu walioendelea walikuwa wanasema wako mbali, wengine wanasema wapo asilimia 80, 90 na wengine wamefikia asilimia 100, nyingine ni nchi ndogo, lakini kwa sababu wana maji ya kutosha, wana mambo mengine wameweza kufikia asilimia 100 ya matumizi ya nishati jadidifu.

|”Sisi wengine bado tuko kwenye safari , bado tunatumia diseli,gesi, kwa mfano sisi Tanzania, Bwawa letu lile (Bwawa la Mwalimu Nyerere) tunatumia Hydro ambayo hiyo, ndiyo nishati Jadidifu , lakini kwa sasa tuseme asilimia 60 ya umeme wetu unatokana na gesi, wanapiga kelele tusitumie gesi, lakini safari, na sisi tumeomba watupe muda zaidi.

***Nishati safia ya kupikia

Rais Samia alisema kama ilivyo agenda yake, alizungumzia suala la nishati safi ya kupikia na kuwatka watuunge mkono kuhakikisha watu wengi Afrika wanapata umeme kutokana na vyanzo vyote hivyo (maji, jua upepe) ili wananchi wapate umeme, waweze kupika kwa kutumia umeme na kupika kwa kutumia nishati safi.

“Na nishati safi hapa sio tu umeme, kuna nishati nyingine mfano pale kwetu Tanzania tunatengeneza mkaa kutokana na vumbi la makaa ya mawe ambao wataalam wamefanya utafiti wameweza kutoa gesi ambazo zina madhara na kufanya mkaa uwe salama.

Kwa sasa hivi unasambaa kwa wingi sana na nishati safi, kwa hiyo ndilo la pili tumezungumzia na kwa bahati nzuri kuna mabenki yanatuunga mkono kwenye nishati safi ya kupikia, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo Afrika, Norway nao wametuunga mkono vizuri sana.

Lakini pia kama mnavyoelewa Januari nchini tutakuwa na mkutano mkubwa wa kuangalia mambo ya umeme, lengo ni ikifika 2030 karibu watu milioni 300 Afrika kati ya watu milioni 700 wawe wanatumia umeme.

“Sasa hivi watu milioni 700 Afrika hawana umeme kabisa, angalau tunataka ikifika 2030 watu milioni 300 wawe wamepata umeme, sasa Mungu akijalia huko nami ninamaliza dhamana hii (Urais) kwa hiyo nitajidai kweli kwamba nimewezesha watu milioni 300 ndani ya Afrika kupata umeme na kwenda kwenye nishati safi ya kupikia ,” alisemaa.

****Jambo la tatu mkutano G20.

Rais Samia alisema kwenye mkutano huo,walizungumzia mambo ya utawala bora na utawala wa sheria.

“Hapo sasa wengine tulikuwa wasikilizaji, lakini yaliyosemwa humo ni haja ya kuona ulimwengu unakwenda salama, haja ya kusimamisha vita vinavyoendelea, haja ya kutoa njia ya kusaidia wale waliofikwa na maafa ya vita na mengine, kuona wanasaidiwaje.

Kwa hiyo wenzetu wenye misuli ndipo walijitutumua kila mtu kusema lake, hatuelewi kama miito ya kusimamisha vita imepokelewaje, hatujui, lakini yalisemwa sasa imetosha, vita visimame na tuone dunia inakwenda kwenye mwelekeo mzuri,” alisema Rais Samia na kuongeza;

“Kwenye mambo hayo hayo makubwa yaliyozungumziwa kwenye mkutano huo na sisi (Tanzania) tunahusika, hatuhusiki na vita, lakini kwenye suala la utawala bora tunahusika kwa sababu kwenye ukanda wetu wa SADC na EAC bado hakuko salama kwa hiyo kama hakuna usalama, ukanda wote ule bado unakuwa kwenye wasiwasi.

***Alama ya saba, ana kwa ana na mataji wa dunia

Rais Dkt. Samia aliweka wazi mafanikio makubwa ambayo Tanzania itapata kutokana na mikutano hiyo ya pembeni (uwili), wakati alipoulizwa kuhusu manufaa ambayo Tanzania itapata kwa kushiriki kwake katika mikutano ya uwili, wakati alipohudhuria Mkutano wa G20 uliofanyika Jiji la Rio di Janeiro.

“Ukiangalia watu niliokutana nao kwenye side meetings (mikutano ya uwili) huwapati kwenye plenary (mkutano wenyewe), unawapata kwenye nikutano ya pembeni ambapo kwa Tanzania tumefaidika sana.” Alieleza Dkt Samia

*** Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa

“Kati ya Marais ambao nilikutana nao ni Cyril Ramaphosa, wa Afrika Kusini. Ambapo kwanza lengo lilikuwa ni kumpongeza kwa uchaguzi wa kwao, ulikuwa mgumu kidogo, lakini alisimama amechagua viongozi wa kufanya nao kazi kuunda Serikali na sasa wanakwenda vizuri.”

Lakini la pili ni kumpongeza kwa kuwa mwenyekiti wa G20 mwakani, jambo kubwa sana maana kwa watu wale ni vigumu kumwamini Mwafrika awe Mwenyekiti wao, ni jambo kubwa sana,” alisema Samia.

Mkutano wa G20 mwaka 2025, unatarajia kufanyika nchini Afrika Kusini chini ya Mwenyekiti ambaye ni Rais wa nchi hiyo, Cyri Ramaphosa ikiwa na kaulimbiu “Kuendeleza Umoja, Usawa, na Maendeleo Endelevu ambayo yote kwa Mwafrika ndio shughuli yetu. Na hivyo kumuhakikishia utayari wa Tanzania kumsaidia katika jukumu lake Uenyekiti wa G20.” Alisema Rais Samia

*** Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Store

Viongozi wengine aliokutana nao ni Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Store, ambapo walijadiliana na kukubaliana kuendeleza mikakati ya kuhakikisha Afrika inapata umeme wa kutosha, kwani Norway ni mshirika mkubwa na muhimu katika masuala ya nishati.

***Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi

Rais Samia pia alikutana na Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi ambapo pamoja na mengi waliyozungumza, mradi wa bwawa la umeme la Mwalimu Julius Nyerere ulijadiliwa, pamoja na mkazo mkubwa kuwekwa katika matumizi mazuri ya maji ya Mto Nile ambapo wanaomba nchi zinazopakana na mto huo kuutumia vizuri ili Misri iendelee kunufaika na mto huo.

*** Waziri Mkuu wa Vietnam

“Nilikutana pia na Waziri Mkuu wa Vietnam tulizungumzia miradi ya pamoja haswa mradi wa Halotel, ambao ulikuwa na matatizo ya hapa na pale , lakini tumemaliza, walikuwa na kesi mahakamani na tumemaliza vizuri na upande wao wanashukuru, lakini pia kuangalia maeneo mengine ya uwekezaji.” Alisema Rais Samia.

***Rais wa Indonesia

Wengine ni Indonesia ambao Tanzania ina ushirikiano katika miradi ya mafuta na gesi ambapo pia wanafuatilia mradi wa LNG, ambapo tayari pia Tanzania ina mikataba ya biashara iliyowahi kusainiwa hivyo kuona jinsi ushirikiano wa kuiendeleza itakavyotekelezwa, lakini pia ziara za wafanyabiashara kuja nchini na kutembelea Indonesia.

“Kwa kuwa Rais wa Indonesia ni Rais mpya ametuhakikishia uhusiano ulioanzishwa na mtangulizi wake utaendelea na kwamba atakapofanya ziara katika nchi za Afrika, atatembelea Tanzana.” Alisema Rais Samia.

***Vigogo WB, AFDB

Katika mikutano hiyo ya pembezoni, Rais Samia pia alikutana na viongozi wa Benki ya Dunia (WB) pamoja na Benki ya Afrika(AFDB) ambapo pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa ni Mkutano wa Nishati unaofanywa kwa kushirikiana na taasisi hizo, utakaofanyika Januari 2025, nchini Tanzania.

“Kwa hiyo tunaangalia mikakati ya kufanikisha hilo. Lakini Benki ya Dunia wametuhakikishia bodi ikishakaa siku zijazo watatupa pesa za miradi mbalimbali ambayo ni pamoja na SGR” alisema Rais Samia

Katika mikutano ya uwili, Rais Samia alikutana na uongozi wa taasisi ya Asia Infrastructure ambayo ni taasisi ya nchi za Asia, ambayo pia wanatoa uanachama kwa nchi nyingine.

“Hivyo Tanzania tumeona umuhimu wa kuingia kwa kuwa benki hiyo inasaidia ujenzi wa miundombinu, fedha za ujenzi wa miundombinu.” Alisema Rais Samia.