April 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ajuza aileza timu ya msaada wa kisheria anavyonyang’anywa urithi kisa kuzaa watoto wa kike

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto

AJUZA Mariam Mahimbo Kolokolo (89) mkazi wa Kijiji cha Manolo, Kata ya Manolo, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ameieleza timu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) kuwa analazimishwa kuondoka kwenye nyumba aliyoachiwa na mume wake baada ya kufariki kwa madai mama huyo alizaa watoto wa kike watupu, watoto 10.

Amedai kuwa wanaoshinikiza ajuza huyo aondoke kwenye mji huo (nyumba zaidi ya moja) ni watoto watano wa kiume wa mke mdogo, mmoja ni askari polisi na mwingine ni mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wanadai dada zao hao wa mke mkubwa, wakiolewa, mji huo utakuwa wa makabila mengine tofauti.

Bibi huyo (Mariam) aliweza kufika kwenye mkutano wa hadhara wa MSLAC uliofanyika kijijini hapo leo Aprili 13 akiwa amefuatana na mtoto wake wa tano Zaharia Rashid Ibura (60) ambaye ndiyo ameweza kutoa malalamiko yake kwa timu ya MSLAC.

Ibura aliwaeleza Wajumbe wa MSLAC kuwa unyanyasaji kwa mama yake mzazi (Mariam) ulianza tangu kwa baba yake mzazi Rashid Ibura (97) ambaye alifariki Mei, 2024, kuwa alioa mke wa pili baada ya kuona mke wake anazaa watoto wa kike watupu.

“Hata kabla ya baba kufariki mwezi Mei, mwaka jana, watoto wa kiume wa baba yetu kupitia mke wake wa pili, ambapo watano ni wanaume na wanne ni wanawake, mmoja ni polisi na mwingine mwanajeshi, wamekuwa wakimtaka mama aondoke yeye na watoto wake wa kike. Wanasema, kwanza wanataka kuendeleza kwa kujenga nyumba, na pili hawataki kuona watoto wa kike wa mke mkubwa wanaolewa na kuishi hapo, wataleta watoto wa makabila mengine.

“Tumejaribu kwenda kushitaki, lakini Wakili Ally Karata aliamua kuja mwaka jana kusuluhisha, na tukaweza kuelewana tena na ndugu zetu, lakini mwezi Machi, mwaka huu, wameanza tena vurugu za kumtoa mama pamoja na sisi watoto wake. Kupitia mawakili wa Mama Samia tuna imani haki yetu itapatikana, na sisi na mama yetu tunabaki pale” alisema Ibura.

Mwananchi mwingine Halima Seif mkazi wa Kijiji cha Manolo aliwasilisha nalalamiko yake mbele ya timu ya MSLAC akidai yeye ni mjane mwenye watoto tisa baada ya mmoja kufariki. Anadai baada ya mume wake kufariki mwaka 2020, akiwa mke wa pili, walijenga nyumba na mume wake huku wakipanda shamba la miti mwaka 1993. Lakini mtoto wa kiume wa mke mkubwa amekuwa akimfuata kwenye shamba hilo huku akimtishia kwa panga, kuwa hataki kumuona.

“Mtoto wa mke mkubwa kila ninapoingia kwenye shamba hilo, aidha kwa kukata kuni au shughuli nyingine, natishiwa kwa panga. Nimekuja kwenye Serikali ya Kijiji, Baraza la Kata, polisi, lakini sijapata haki yangu. Hivyo Mama Samia kupitia watu aliowatuma naomba anisaidie nipate haki yangu” alisema Seif huku akionesha rundo la nyaraka kila alikopita.

Naye mkazi wa Kijiji cha Manolo Makelo Jambia aliwasilisha malalamiko yake kwa MSLAC kuwa kuna eneo alilitumia Mwekezaji wa kzungu anaitwa Herman Mufi kama kiwanda cha kuchakata mbao, baadae akafanya gereji ya magari, ila alipofariki mwaka 1978, eneo hilo lenye ekari 10 wakajimilikisha watu wachache na kuanza kuwakodisha mashamba, hivyo wanamuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kubatilisha umiliki wake.

“Tunataka eneo hilo tuweke soko, mnada na shughuli nyingine za umma. Soko lililopo hapa Manolo lipo kwenye mkondo wa bonde la maji, mvua zikinyesha ni hatari kwa watumiaji wa soko. Kuna siku watu wakiwa sokoni waliepua miili ya watu wawili waliosombwa na maji huko juu wakaja kuonekana hapa sokoni. Tuna imani Mama Samia atasikiliza kilio chetu.

“Na nataka kumpongeza. Mimi nikiwa mzee wa miaka 70 sijawahi kuona Rais kama Samia. Ameweza kugharamia mawakili na watu wa kada mbalimbali ili kuja kusikiliza kero za wananchi. Nataka kusema, wananchi wanateseka na wanakufa kutokana na kero mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi na kunyanyaswa, lakini kwa kuja hawa ndugu zetu tutapona” alisema Jambia.

Ofisa Ardhi Wilaya ya Lushoto akiongoza timu ya MSLAC Adam Pascal alisema wananchi wa Kijiji cha Manolo hawahitaji Wakili ili kupata eneo hilo alilokuwa anamiliki Mwekezaji wa kigeni, bali wanatakiwa kukaa kikao cha Serikali ya Kijiji baadae Baraza la Maendeleo la Kata (WDC), kisha Baraza la Madiwani, na baadae TAMISEMI kwa ajili ya kuomba kupewa eneo hilo ili wafanyie matumizi mengine.

Wakili wa Kujitegemea wa MSLAC wilayani Lushoto Ally Kimweri alisema  mgogoro wa familia ya Mariam Kolokolo anaufahamu sababu uliwahi kufika mahakamani, na baadae uliondolewa ili ukaweze kupatiwa ufumbuzi kwa usuluhishi wa kindoa.

“Wale vijana wa kiume wanatumia ubabe kutaka kuwanyang’anya lile eneo watoto wa mke mkubwa ambao wote ni wanawake. Ukizingatia ndani yao kuna mmoja ni askari polisi na mwingine askari wa JWTZ, wanasema hawataruhusu watoto wa kike kuishi pale. Lakini baba yao mwaka 2008 alishagawa eneo la mke mkubwa na mke mdogo. Lakini watoto walivyomuona baba yao amechoka, wakaanza kuwapelekesha wale watoto wa kike kutaka kuwanyang”anya eneo lao” alidai Kimweri.