Na Daud Magesa, TimesMajira Online, Mwanza MFANYABIASHARA Emmanuel Nyambela (40) Mkazi wa Bwiru Msikitini Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, jijini Mwanza,amejiua kwa kujipiga risasi kifuani upande wa kushoto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbroad Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari,leo amethibitisha tukio hilo la mfanyabiashara huyo kujiua.
Amesema tukio hilo lilitokea eneo la Bwiru Msikitini, Aprili 16, mwaka huu, majira ya saa 3:45 usiku, baada ya Nyambela kujipiga risasi kifuani upande wa kushoto akitumia silaha aina ya bastoa aliyokuwa akiimiliki.
Mutafungwa amesema mfanyabiashara huyo anadaiwa kujiua kwa kujipiga risasi kutokana na msongo wa mawazo uliosababishwa na mgogoro wa kifamilia baada ya kutoridhishwa na mgawanyo wa mali.
Amesema kuwa alitumia bastola yake aina ya TZCAR 80190 yenye namba za usajili KCAL 38 yenye uwezo wa kubeba risasi 9 lakini hakuna madhara kwa watu wengine wa familia hiyo yaliyosababishwa na marehemu huyo zaidi ya kujitoa uhai wake.
Kamanda huyo wa polisi alitoa rai kwa jamii inapokumbana na changamoto ya migogoro ya kifamilia suluhisho si kujitoa uhai bali wawaone viongozi wa dini,wataalamu wa saikolojia na ushauri nasaha ili wawanasihi.
Mutafungwa pia ametumia fursa hiyo kuwaonya na kuwataka madereva wa vyombo vya moto kuacha kuendesha magari wakiwa wamelewa,wazingatie na kuheshimu sheria za barabarani na kuepuka kutumia vilevi wakati wa sikukuu ya Idd El Fitri.
Aidha aliwataka wazazi kuchukua tahadhari na kuhakikisha wanakuwa waangalifu kwa usalama wa watoto na kuepuka kuwaacha wenyewe wakati wa sikukuu.
Pia kutokana na matukio ya uhalifu kipindi cha sikukuu ya Idd El Fitri aliwashauri wananchi kutoacha nyumba wazi bila uangalizi ikitoa dharura ni vema washirikishe majirani ingawa jeshi la polisi limejipanga na litahakikisha usalama wa raia unakuwepo muda wote wa sikukuu.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria