March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Airtel Tanzania yaadhimisha wiki ya Huduma kwa Wateja 2025

Na Mwandishi Wetu Timesmajira Online

KAMPUNI ya Airtel Tanzania imeungana na mataifa mbalimbali duniani kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka 2025, ikiendana na kaulimbiu ya kimataifa “Mission Possible” (Dhamira Inawezekana) Kauli mbiu hii inalingana moja kwa moja na falsafa ya kampuni hiyo ya “Mteja Kwanza”, ambayo imekuwa dira ya maamuzi na mwelekeo wake katika kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya kuthibitisha dhamira ya kampuni kuboresha huduma, kukuza ubunifu na kuongeza thamani kwa wateja wake.

“Kwa Airtel, ‘Mission Possible’ ina maana ya ‘Mteja Kwanza’. Tunaichukulia wiki hii kama fursa ya kuimarisha utamaduni wetu wa kumweka mteja mbele ya kila kitu. Tutadhihirisha hilo kupitia vituo vyetu vyote vya huduma, idara za huduma kwa wateja na timu ya uongozi,” amesema Kamoto.

Ubunifu na Uboreshaji wa Huduma

Katika mwaka uliopita, Airtel Tanzania imewekeza kwenye huduma bunifu zinazorahisisha maisha ya wateja. Huduma ya LUKU Token Retrieval imewasaidia maelfu ya wateja kupata namba zao za LUKU kwa urahisi na kuepusha usumbufu wa kukatika kwa umeme. Vilevile, zana za kujitegemea (self-care tools) zimewapa wateja uwezo wa kusimamia akaunti zao kwa uhuru na haraka.

Kampuni pia imeimarisha mifumo ya kupokea mrejesho kutoka kwa wateja ili kuelewa mahitaji mapya na kuboresha huduma kulingana na matarajio yao. Hatua hii imeenda sambamba na upanuzi wa mtandao wa vituo vya huduma nchini kote, mijini na vijijini.

“Katika kipindi hiki, tumeandaa shughuli mbalimbali za kuwashukuru wateja kupitia maduka yetu na majukwaa ya kidijitali, kama ishara ya kutambua uaminifu wao kwetu,” ameongeza Bw. Kamoto.

Huduma za Kujihudumia Zaongezewa Nguvu

Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Airtel Tanzania, Adriana Lyamba, amesema kampuni imeboresha zaidi huduma zinazompa mteja uwezo wa kujihudumia kwa urahisi, usalama na ufanisi.

Miongoni mwa huduma hizo ni self-reversal, inayomruhusu mteja kurejesha muamala wa Airtel Money uliofanyika kimakosa bila kutembelea wakala au ofisi.

“Huduma hii inampa mteja uwezo wa kurekebisha makosa papo hapo na kudhibiti akaunti yake kikamilifu,” amesema Bi. Lyamba.

Dhamira Endelevu

Airtel Tanzania imesisitiza kuwa falsafa ya “Mteja Kwanza” si kauli ya kimasoko pekee, bali ni msingi wa utoaji huduma, ubunifu na uboreshaji wa maisha ya wateja wake kila siku.