Ashura Jumapili TimesMajira online Kagera
Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba imemuhukumu Emmanuel Barakanfitiye maarufu kama rais (52) mkazi wa kitongoji cha Karundi A kijiji cha Mwanga Wilaya ya Biharamlo mkoani Kagera, kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji ya mama yake mzazi ( 75 ).
Katika kesi hiyo Jamhuri iliwakilishwa na Mwakili wawili ambao ni Matrida Assey pamoja na Gloria Lugeye.Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba Lilian Itemba Mei 26 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari,Wakili wa Serikali Matrida Assey,amesema mshitakiwa huyo amehukumiwa baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili ambao umemtia hatiani na kumuhukumu kifungo cha kunyongwa hadi kufa.
Amesema tukio hilo la mauaji ya Mariana Matabaro ( 75 ) lilitokea Mei 13, 2020 ambapo aliuawa na mtoto wake wa kumzaa Emmanuel akishirikiana na mshitakiwa wa pili Jackson Emmanuel (21) ambaye marehemu ni bibi yake ambaye wakati wa tukio alikuwa na miaka16.
Assey akizumgumzia tukio hilo alitaja sababu ya mauaji hayo kuwa ni mgogoro wa ardhi kati ya marehemu na mtoto wake huyo.
Amedai kuwa, mashuhuda ambao pia ni watoto wawili wa marehemu akiwemo Mambo Barakanfitiye na George Barakanfitiye ambao wanaishi hatua 10 kutoka kwenye nyumba alipokuwa anaishi mama yao, siku ya tukio saa 2:00 usiku walikuwa wamekaa nje wanaota moto wakasikia kelele.
“Kelele zilikuwa ni za mama yao za kuomba msaada, anaita nisaidie,nisaidie wakati wanasikia kelele ghafla walimuona mama yao anatoka ndani anakimbia kuelekea kwenye nyumba za hao watoto wake” amesema Wakili Assey.
Ameongeza kuwa, wakati watoto hao wanaota moto walikuwa na tochi hivyo waliposikia kelele wakaanza kumulika na kumuona kaka yao ambaye ni Emmanuel akiwa na mtoto wake Jackson na mtu mwingine ambaye hawakumtambua kwa sababu alikuwa amejificha wakiwa wanamfukuza marehemu.
“Wakati anawamulika walikuwa karibu Mambo akataka kwenda kumsaidia, kabla hajaenda akamuona Emmanuel akiwa ameshika panga na kumkata mama yake kichwani.Mshitakiwa wa pili Jackson akachukua jiwe na kumpiga nalo Mambo kifuani na mkononi akadondoka chini akawa ameshindwa kutoa msaada kwa marehemu.Goerge alipoona Mambo ameishapigwa na wenzake wanasilaha akaogopa akakimbia anapiga kelele kuita watu waje kutoa msaada,” amesema Wakili Assey.
Amesema wakati Mambo, akiwa amelala chini alikuwa anaona mama yake anaendelea kushambuliwa kwa mapanga na alipojaa damu wale wauaji waliondoka na baadaye walirudi na kuhakikisha amekata roho na Goerge ambaye alikimbia alipiga simu kwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Karundi A Petro Bukuku.
Baada ya Mwenyekiti kupata taarifa hizo alifika eneo la tukio na kupiga simu kituo cha Polisi Biharamlo ambapo usiku huo wananchi waliendelea kulinda mwili na wengine walienda kuwatafuta wauaji.
Amesema walipofika kwa mke mdogo wa Emmanuel,aliwambia alifika nyumbani akiwa na wasiwasi akaondoka na walivyoenda kwa mke mkubwa wa Emmanuel kumuulizia Jackson alisema hayupo nyumbani ameondoka.
Aidha wauaji hao baada ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani mtuhumiwa wa kwanza Emmanuel alitiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa huku Jackson ambaye wakati anatenda kosa alikuwa ni mtoto hivyo atakaa gerezani mpaka atakapotoka kwa msamaha wa Rais.
More Stories
Kiongozi wa Mwenge awataka RUWASA kukamilisha mradi wa maji kwa wakati Kilindi
Balozi Nchimbi aongoza waombolezaji kumuaga Mzee Mongella
Sheikh Kabeke asisitiza maadili na amani kuelekea uchaguzi 2025