March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afya ya Uzazi bado changamoto kwa Wasichana wa Rika Balehe

Na Penina Malundo,Timesmajira

WASICHANA wengi wa rika balehe nchini bado wanakabiliwa na changamoto kubwa za afya ya uzazi zinazohatarisha maisha yao, elimu na mustakabali wa ndoto zao.

Taarifa zinaonyesha kuwa baadhi ya wasichana hukosa elimu ya kutosha kuhusu mabadiliko ya miili yao, jambo linalowafanya washindwe kujitunza wakati wa hedhi.

Wengi hulazimika kukatisha masomo kwa siku kadhaa kila mwezi kutokana na uhaba wa vifaa vya kujihifadhi, hali inayosababisha kushuka kwa ufaulu na kuathiri ushiriki wao shuleni.

Aidha,ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi umekuwa kichocheo cha mimba za utotoni na maambukizi ya magonjwa ya zinaa kwani Wataalamu wa afya wanasema mimba za mapema husababisha wasichana wengi kuacha shule, huku baadhi wakijikuta kwenye matatizo makubwa ya kiafya wakati wa kujifungua kutokana na miili yao kutokuwa tayari.

Mbali na hilo, tatizo la ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia limeendelea kuwa kikwazo kikubwa. Mashirika yasiyo ya kiserikali yameendelea kusisitiza umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi kuanzia shule za msingi, huku yakihimiza serikali kuwekeza zaidi vifaa vya kujihifadhi wakati wa hedhi na kuboresha upatikanaji wa huduma rafiki za afya kwa vijana.

Kulingana na Ripoti ya Tanzania Demographic and Health Survey (TDHS) ya Mwaka 2022,inaonesha kuwa asilimia 22 ya wanawake wa umri kati ya miaka 15–19 wameshakuwa na mimba au ni wajawazito ,kati yao,asilimia 16 wametoa mtoto na asilimia 6 ni wajawazito wakati wa utafiti.

DHS ProgramRipoti ya UNFPA inaonyesha pia kwamba kiwango cha uzazi kwa wasichana,utafiti mmoja unaonyesha kuwa asilimia 27 ya wasichana wa bara la Tanzania wamekuwa na mtoto au wakiwa wajawazito, ikilinganishwa na Zanzibar ambapo idadi ni asilimia 8. BioMed CentralKwa mujibu wa data ya “Child Marriage Data Portal”, asilimia 29 ya wanawake wa umri kati ya miaka 20-24 wanatajwa kuwa wameolewa au kuingia katika muungano kabla ya kufikia umri wa 18 nchini Tanzania.

Child Marriage Data Portal Mtaalam wa masuala ya Afya ya Uzazi kutoka Shirika-mtandao la vijana lililo jikita katika kuimarisha taarifa- (GenACT-Africa),Mathias Kapenda anasema suala la Afya ua Uzazi ni mtambuka ambalo inahusisha usalama wa ujauzito,kujikinga magonjwa ya ngono na kupata taarifa ya kujua mwili,kufahamu mabadiliko ya mwili na wakati gani mtoto wa kike anaweza kupata mtoto au wakati gani asiweze kupata mtoto.Kapenda anasema afya ya uzazi imekuwa inawaathiri wasichana rika balehe kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo suala la changamoto ya magonjwa ya ngono kwa vijana.

”Kijana hakikosa taarifa na elimu ya kujikinga na magonjwa ya ngono,matumizi ya njia salama ya kujikinga na maambukizi hivyo kusababisha vijana wengi kuathirika na magonjwa ya ngono au zinaa.

”Kuna umuhimu mkubwa wa kusikiliza majibu haya kwani yanafundisha namna ya utumiaji wa masuala ua afya ya uzazi wa Mtu kutojua maendeleo ya mwili na hisia kunakuwa na mabadiliko mbalimbali kwa mfano msichana kujua kipindi chake cha hedhi.

”Pia suala hili linaathiri sana mimba za utotoni,kukosekana kwa elimu na afya ya uzazi kwa ujumla imepelekea vijana wengi hasa mabinti kuingia katika mimba za utotoni hii ni changamoto kubwa,”anasema Kapenda.

Anasisitiza kuwa vijana kukosa haki na ulinzi wa taarifa zao nayo ni miongoni mwa maamuzi ambayo mabinti wengi wanakuwa hawawezi kujiamini kwa sababu taarifa zao zinakuwa sio siri tena akizungumza na mtaalamu wa afya inakuwa sio siri tena.

”Sisi kama wadau wa masuala ya Afya ya Uzazi tusichoke kuendelea kutoa taarifa na huduma mbalimbali katika jukwaa la vijana katika kueleza changamoto walizokutana nazo,”anasema.

Kwa upande wake Dkt.Mashingo Lerise Mtaalam Masuala ya Afya ya Uzazi anasema njia za za uzazi wa mpango zinasaidiaje kwa kiasi kikubwa kupanga uzazi uliosalama.

Anasema uzazi wa mpango kwa vijana ni dhana ambayo imejaa upotoshaji mwingi kutokana na elimu sahihi kutowafikia kwa wakati, hivyo wanalazimika kufuata elimu ya upotoshaji wanayokutana nayo mitaani na mitandaoni.

Anasema vijana wanatafuta taarifa ila hawajajua wanazitafutia wapi,maeneo mengi ambapo wanatafuta hizo taarifa sio sahihi na taarifa wanazozipata haziwasaidii bali zinawapoteza.

“Vijana wanapaswa kutumia wataalamu wa afya na sio kupata taarifa Mitaani wanazoambiana na marafiki zao hiyo inakuwa ni hatari kwao kupata taarifa za upotoshaji kwa njia ya haraka na kuwafanya kushindwa kutumia njia hizo za uzazi wa mpango,”anasema na kuongeza

“Serikali imesambaza wataalamu ambao wamepewa mafunzo maalum ya kutoa elimu ya rika balehe na kwa vijana kwa ujumla kupewa huduma rafiki ili wanapotafuta taarifa wawe wanazipata kwa wakati ili kuepuka vishawishi na kuingia kwenye hatari za kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi ,”anasema.

Anasema kwenye vituo vya afya kwa sasa kondomu zinagawiwa bure lengo ikiwa kumlinda kijana ,au mtu alieanza kushiriki tendo la ngono kujilinda kuepukana na magonjwa ya zinaa ikiwemo magonjwa ya homa ya ini.