November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afungwa jela miaka 60 kwa kubaka mwanafunzi

Na Jumbe Ismally, Igunga

MAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora imemuhukumu kifungo cha miaka 60 jela, Machibya Shija, baada ya kupatikana na kosa la kubaka mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 16.

Mahakama hiyo imetoa adhabu hiyo mwishoni mwa wiki baada ya mshtakiwa huyo kukiri makosa yake mawili yaliyokuwa yakimkabili katika Mahakama.

Awali mtuhumiwa huyo alikiwa akikabiliwa na shtaka la kumbaka mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Bukoko.

Adhabu hiyo ilitolewa na Hakimu, Eddah Kahindi. Hakimu Kahindi amesema kwa hiari yake mwenyewe mshtakiwa alikiri kutenda makosa yake yote mawili bila kulazimishwa.

Hakimu Kihindi amesisitiza kwamba baada ya ushahidi huo ulionyooka, Mahakama hiyo bila shaka yoyote ile inamtia hatiani mshtakiwa huyo kwa kutenda makosa hayo yote mawili kinyume na sheria.

Kabla ya hukumu hiyo Mwendesha Mashtaka wa Polisi aliiomba Mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo kwa kuwa vitendo, hivyo pamoja na Serikali kuvikemea,lakini bado vimekuwa vikijirudiarudia mara kwa mara.

Akitoa hukumu hiyo, Kahindi amesema kwamba Mahakama hiyo inamuhukumu Shija kwenda kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kila kosa na kwamba kwa makosa yote mawili, atatumikia miaka 60 ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Awali Kataya alidai kwamba mshtakiwa Machibya Shija anakabiliwa na mashtaka mawili na kwamba katika shtaka la kwanza ni la kubaka mwanafunzi kinyume na kifungu 130 (1)(2)( c) pamoja na kifungu (131)(1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2019 inayozuia kutenda makosa kama hayo.

Katika shtaka la pili lililikuwa la kumzuia mwanafunzi kutoendelea na masomo yake.

Anadaiwa kutenda makosa hayo Novemba 5,mwaka huu, majira ya saa za usiku katika Kijiji cha Mangungu,Kata ya Bukoko.