Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online
MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, ametoa msimamo wa chama hicho kuhusu mgombea urais wa chama hicho, Benard Membe, huku akimtaka asiwachanganye wanachama wa chama hicho.
Maalim Seif alitangaza msimamo wa chama hicho ikiwa ni siku mbili tangu, Membe azungumze na waandishi wa habari na kutangaza msimamo wake kwamba yeye bado mgombea halali wa chama hicho na anaendelea na kampeni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Maalim Seif amesema anasikitika kwa kauli iliyotolewa na Membe jana (juzi), kwani ACT-Wazalenzo kupitia Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho, walikubaliana kwamba yanahitajika mabadiliko katika nchi yetu.
“Kwa hiyo tulikubaliana kwamba kama vyama makini havitashirikiana itakuwa vigumu kuiondoa CCM, hivyo ulitoa mamlaka kwa vikao vingine vya chama kuhakikisha ACT inafanya kila juhudi kushirikiana na vyama makini kwenye uchaguzi wa mwaka huu,”amesema Maalim Seif.
Amesema hadi sasa hakuna taarifa yoyote kwamba kuna mwanachama anapinga msimamo wa chama hicho kushirikiana na CHADEMA. Aliongeza kuwa kutokana na uamuzi huo ndani ya chama, hakuna mpasuko kama Membe anavyotaka ionekane hivyo kwa wanachama.
“Wanachama wa ACT-Wazalendo wanajua lengo lao, kwamba wanataka CCM ikae upande (iondoke). Kama kuna mtu anataka CCM iendelee, basi ndiye kama hao (akina-Membe) wewe kama mjumbe wa Kamati ya Uongozi utakataaje maamuzi ambayo ulishiriki?”Amehoji Maalim Seif na kuongeza;
“Je umeletwa ACT-Kwa lengo maalum! Sisi tupo macho na upinzani mara hii ni imara na upo tayari kuiondoa CCM, kwa hiyo hata msimamo wa chama hatujasema tunawaunga mkono wagombea wote wa CHADEMA na wala wao hawajasema wanaunga mkono wagombea wote wa CHADEMA, hiyo ipo kwenye vichwa na yapo baadhi ya majimbo wamekubaliana wao wenyewe kuachiana majimbo.”
Amesisitiza kwamba ndani ya ACT-Wazalendo hawana mpasuko ni chama kimoja, labda kama Membe anawajua wenzake, lakini hakuna mpasuko ni chama kimoja chenye lengo moja.
Amefafanua kwamba Membe alipojiunga na ACT walimwambia kwamba maazimio ya Mkutano Mkuu ni kushirikiana na vyama vingine makini vya upinzani na kwamba yeye amekubaliana na hilo, lakini leo hii inashangaza kusikia anasema anaendelea na kampeni.
“Je, hizo kampeni zake mmeziona? Baada ya kuona kampeni zinakwenda takribani mwezi mmoja na nusu za kwake zimesuasua tulikutana katika Kamati ya Uongozi na kushauriana na Membe akiwepo.
Tulishauriana kwamba mgombea wetu haonekani, afadhali ya mzee wa ubwabwa (Hashim Rungwe) anaonekana. Membe anasema ikifika tarehe fulani hajaanza kampeni waanze kumuunga mkono Lissu,” alizidi kueleza Maalim Seif..
Amesema Kamati ya Uongozi baada ya kuona hiyo tarehe waliyokubaliana imefika kabla Membe hajaanza kampeni, walikubaliana kumuunga mkono Lissu.
Amefafanua kwamba anachosema Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo (Zitto Kabwe) ndiyo maamuzi ya chama ya vikao halali.
Amezidi kusema kwamba inasikitisha kuona mjumbe wa kamati hiyo anakana maamuzi ya chama. “Mimi kama Mwenyekiti wa chama moja ya majukumu yangu ni kusimamia maamuzi ya chama, kwa hiyo maamuzi yaliyotolewa na vikao hivyo ni jukumu langu kuyasimamia,” amesema na kuongeza;
“Kikao cha juu kilishasema tushirikiane na wenzetu kwa hiyo lazima nisimamie hayo maamuzi. Kwani tulikubaliana tushirikiane kumuunga mkono mgombea mwenye uwezekano wa kumshinda Magufuli (Rais Magufuli) na hii inaonekana wazi.”
Kwa hiyo amesema aliyosema Zitto wala yeye (Seif) sio yake, bali ni maamuzi ya chama na kwamba ni lazima wanachama waheshimu maamuzi ya vikao vya chama.
“Afanye kampeni zake tuone, nia zake ni kwenda kuwachanganya Watanzania na ukweli ni kwamba mgombea anayeenda kushinda ni Lissu na ninasema waziwazi kwamba namuunga mkono Lissu.
Hapa tunasubiri barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mrema (Augustino) anaposema anamuunga mkono Magufuli, hakuandikiwa barua, Cheyo amesema hivyo ikawa kimya, lakini niliposema mimi namuunga Lissu mkono nikaandikiwa barua,” amesema Seif.
Amesema mgombea wa CHAUMA alitangaza kumuunga mkono Maalim Seif Zanzibar, siku ya pili wakaandikiwa barua msajili akihoji kwa nini wanakubali kuungwa mkono na chama kingine.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza