January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ACT Wazalendo yampongeza Rais Samia mradi wa EURO mil. 457

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

CHAMA Cha ACT Wazalendo, kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuisaidia Zanzibar kupata Euro milioni 457 kwa ajili ya utekelezaji mradi wa kimkakati wa Barabara ya Mkoani/Chakechake, Uwanja wa Ndege Pemba, Barabara ya Tungu- Makunduchi na Kisauni-Fumba

Kwa mujibu wa chama hicho ujenzi  wa mradi huo ulikwama kutokana na kiongozi mmoja kutaka kupewa kamisheni yake ili kupitia mradi huo.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wzalendo, Ismail Jussa, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Geji Bububu Mkoa wa Mjini Magharib Unguja.

Amesema mradi huo wa kimkakati ulikuwa ujenge barabara ya Mkoani/Chakechake, Uwanja wa Ndege Pemba, Barabara ya Tunguu/ Makunduchi na Kisauni/Fumba kwa kutumia mkopo uliodhaminiwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Uingereza.

Jussa amesema kujengwa kwa kiwanja cha ndege cha kisasa Pemba pamoja na barabara ya Chakechake kungefungua kiuchumi kisiwa hicho, lakini mradi huo ulikwama tangu Novemba 2023 na kampuni ya MECCO ndiyo iliyoshinda zabuni.   

“Kampuni ya Parpov na Mecco ndio waliokuwa watekelezaji wa mradi huo na mikataba ilikuwa imesainiwa, lakini alitokea kiongozi mmoja akawa anadai rushwa kupitia fedha za mradi huo, na Mecco kuamua kwenda kufungua kesi Mahakamani,” amesema.

Akizungumzia ubinafsishaji wa Shirika la Bandari Zanzibar tangu kukabidhiwa wawekezaji kutoka Ufaransa, Jusa amesema hakuna uboreshaji wowote wa huduma zaidi ya gharama za uzalishaji kuendelea kupanda na kuwaumiza wananchi wa Zanzibar.

Amesema kwa mujibu wa bajeti ya matumizi na mapato ya wizara ya ujenzi, mawasiliano na usafirishaji ya mwaka wa fedha 2024/2025 imesema shirika hilo linakusudia kukusanya mapato ya sh. bilioni 37 wakati matumizi yake ni sh. bilioni 77 kwa mwaka.

Amesema waziri mwenye dhamana alisema Serikali inatarajia kukopa sh. bilioni 40 na kuwakabidhi shirika la bandari jambo ambalo ni kuongeza madeni kwa Serikali na hakuonekani faida yoyote tangu shirika kubinafsishwa.

Aidha, amesema kwamba mradi wa ujenzi wa jengo la pili la abiria wa uwanja wa Abeid Amani Karume ambao umepanga kutumia dola milino 30 unafanyika kinyume na sheria kwa sababu fedha haziaidhinishwa na baraza la wawakilishi na hakuna zabuni iliyotangazwa jambo ambalo ni kinyume na sheria ya zabuni na sheria ya ushindani ya kumlinda mlaji.

Naye Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud, amesema viongozi na watumishi wanaotuhumiwa kuhusika na ubadhilifu na mikataba ya kifisadi lazima watafunguliwa mashtaka baada ya ACT kushika madaraka mwaka 2025.

“Rasilimali za nchi hii zinatakiwa zitumike inavyotakiwa, kama umeiba kukufunga tutakuja kukufunga sisi maana tunajua nyie wenyewe hamuwezi kufungana lakini sisi tunawaambia aliehujumu mali ya serikali,alieingia mikataba ya kifisadi, aliekwapua kila pahala mkono wake tutaukata tutahakikisha anafikishwa kwenye vyombo vya sheria na atakaethibitika atafungwa, mie mwenyewe nimedumu katika vyombo vya sheria kwa miaka 18” amesema Othman ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa mashtaka Zanzibar.