Na.Mwandishi wetu,Timesmajira
WAWAKILISHI i wa Chama cha ACT Wazalendo katika Baraza la Wawakilishi wameiitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu gharama halisi za ujenzi wa miundombinu inayohusiana na maandalizi ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, wakieleza kuwa kauli zinazotolewa na viongozi wa Serikali zimeibua sintofahamu miongoni mwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Zanzibar, Mnadhimu wa ACT Wazalendo katika Baraza la Wawakilishi, Profesa Omar Fakih Hamad, amesema chama hicho kimebaini kuwepo kwa tofauti kubwa za taarifa zilizotolewa na Serikali kuhusu kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, jambo ambalo linahitaji ufafanuzi wa haraka.
Amesema katika hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Fedha na Mipango aliliambia Baraza la Wawakilishi kuwa Serikali imetenga shilingi trilioni 1.69 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya michezo, usafiri, utalii na huduma za kijamii kuelekea AFCON 2027.
Hata hivyo, baadaye Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa gharama za miundombinu hiyo ni takribani shilingi bilioni 300, huku Waziri huyo akitoa ufafanuzi mwengine akisema kiwango sahihi ni shilingi trilioni 1.069.
Kwa mujibu wa ACT Wazalendo, tofauti hizo zimezua maswali kuhusu taarifa ipi ndiyo sahihi na ni kwa nini Serikali imetoa maelezo yanayokinzana katika suala ambalo lina athari kubwa kwa matumizi ya fedha za umma.
Chama hicho kimesema wananchi wana haki ya kufahamu gharama halisi za mradi huo, vyanzo vya fedha, mgawanyo wa fedha kwa kila mradi pamoja na masharti ya mikopo inayotarajiwa kugharamia sehemu ya utekelezaji wa miundombinu hiyo.
Aidha, ACT Wazalendo imeeleza wasiwasi wake kuhusu uendelevu wa uwekezaji huo baada ya kumalizika kwa mashindano ya AFCON 2027, kikitaka Serikali kuweka wazi mpango wa matumizi ya miundombinu hiyo ili kuhakikisha inaleta manufaa ya muda mrefu kwa uchumi wa Zanzibar.
Pia chama hicho kimeitaka Serikali kueleza iwapo kulikuwa na makosa katika uwasilishaji wa taarifa za bajeti, chanzo cha makosa hayo pamoja na hatua zilizochukuliwa, huku kikisisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.
Katika taarifa hiyo, ACT Wazalendo imeitaka Serikali kutoka na kauli moja rasmi kuhusu gharama kamili za miundombinu ya AFCON 2027 kwa Zanzibar, ikisema ufafanuzi huo utasaidia kuondoa taharuki iliyojitokeza na kurejesha imani ya wananchi kuhusu usimamizi wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani, Mohammed Ali Salim, amesema ACT Wazalendo haipingi ujenzi wa miundombinu ya AFCON 2027, bali kinachoibua wasiwasi ni tofauti za takwimu na taarifa zinazotolewa na Serikali kuhusu gharama za miradi hiyo.
Amesema kauli zinazotolewa na viongozi wa Serikali zinaonesha kutokuwepo kwa msimamo mmoja, jambo linalozua maswali iwapo Serikali imekuwa makini katika kutoa taarifa kwa umma au kama bajeti zinazowasilishwa hazioneshi uhalisia wa matumizi yaliyokusudiwa.
“Hili linatupa mashaka kwa sababu taarifa hizi zinatolewa na wasemaji wa Serikali, rais amesema jambo moja, Waziri wa Fedha amesema jambo jengine, hivyo wananchi wana haki ya kupata ufafanuzi kuhusu ipi ndiyo taarifa sahihi,” amesema Mohammed.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Ole, Seif Suleiman Seif, amesema kiwango cha fedha kinachotajwa kutumika katika miundombinu ya AFCON hakilingani na hali halisi ya uchumi wa Zanzibar.
Amesema hoja yao inatokana na ukweli kwamba Zanzibar si mwanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) wala Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), na pia si muandaaji rasmi wa mashindano hayo.

More Stories
Sangu :Wadau tuchangie madawati
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yamkabidhi Tuzo Rc.Babu
Miaka 30 Jela kusafirisha mirungi kilo 75.15