May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ACT-Wazalendo waadhimisha miaka 9, kwa upandaji miti

Na Mwandishi wetu, timesmajira

CHAMA cha ACT Wazalendo katika kuadhimisha miaka tisa ya Chama hicho,kimekusudia kuwa na mpango wa kuhamasisha uhifadhi na ulinzi wa Mazingira kwa viongozi, wanachama na jamii kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu katika siku ya kwanza ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa ACT Wazalendo alisema chama chao kilichopata usajili wa kudumu Mei 5,2014 ambapo Mwaka huu kinaadhimisha , kutimiza miaka tisa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kichama kwa siku tatu kuanzia Mei 3 hadi 5, 2023 katika Mkoa wa Pwani.

“Leo wanachama na viongozi wa Chama chetu nikiongoza na Mimi mwenyewe,Katibu Mkuu Ado Shaibu tumepanda miti na kufanya usafi wa mazingira kwenye zahanati ya Mwandege katika Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani,”amesema.

Akizungumza baada ya shughuli hiyo,Ado amesema wameamua kuyatumia maadhimisho ya miaka tisa ya ACT Wazalendo kupanda miti ili kushiriki katika utunzaji wa mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na mabadiliko ya tabia nchi. Madhara yake yameonekana kwenye sekta mbalimbali hasa za kilimo, nishati, utalii na maji. Uzalishaji wa chakula na umeme unashuka kila mwaka kwa sababu ya uhaba wa mvua” amesema na kuongeza,

“Ukiacha rai mbalimbali tunazotoa kwa Serikali kama vile kununua chakula cha ziada ili kukabiliana na mfumuko wa bei za vyakula na kutafuta vyanzo mbadala vya nishati ili kukabiliana na mgao wa umeme ambayo ni madhara ya moja kwa moja ya mabadiliko ya tabia nchi tumeona pia tushughulike na kiini cha tatizo kwa kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa vitendo. Ofisi ya Katibu Mkuu kwa kushirikiana na Msemaji wa Kisekta wa Mazingira, itakuja na Mkakati maalum wa kuwahimiza viongozi wa ngazi zote, wanachama na wananchi kwa ujumla kupanda miti na kuyatunza mazingira”amesema Ado.

Shughuli za maadhimisho ya miaka hiyo ya ACT Wazalendo zitaendelea kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii katika Jimbo la Mkuranga ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa , Makamu Mwenyekiti wa Chama Bara,Dorothy Semu ambapo
kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kuwa kuwa Mei 5 Mwaka huu.