Na Mwandishi wetu
Chama cha ACT Wazalendo kimesema kimejipanga kuuteka kisiasa Mkoa wa Dar es salaam kwa kujiimarisha katika Mitaa yote 365, Kata zote 102 na Majimbo yote 10 ya Mkoa huo.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo,Ado Shaibu kwenye ziara yake katika Jimbo la Segerea leo tarehe 14 Novemba 2023.
Kwenye ziara yake, Katibu Mkuu amekutana na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo hilo ambao ni viongozi wa Kata zote 13 za Jimbo hilo.
Kwenye hotuba yake Ndugu Ado amesema kuwa ACT Wazalendo, kwa mwaka mzima kimejikita katika kufanya kazi za chini katika Mkoa wa Dar es salaam na mikoa mingine Nchini na kwamba mafanikio yaliyofikiwa katika Jimbo la Segerea katika uchaguzi wa ndani ni ishara za matunda ya kazi hiyo.
“Ninawapongeza sana viongozi wa Segerea kwa kukamilisha uchaguzi kwenye Kata zote 13 na Mitaa yote 62 ya Jimbo la Segerea. Nia yetu ni kuuteka kisiasa Mkoa wa Dar es salaam. Segerea mmeonesha mfano mzuri katika kufanikisha hilo” amesema Ado.
Katika hatua nyingine,Ado amesema kuwa viongozi wa Chama hicho kwa kushirikiana na vyama vingine vya siasa na wadau wa demokrasia kwa ujumla wake wanapambana kuhakikisha kuwa chaguzi zijazo Nchini zinakuwa za haki, huru na za kuaminika.
More Stories
Nani kuwa mrithi wa Kinana CCM?
Watendaji Songwe wapatiwa mafunzo uboreshaji daftari la mpiga kura
Samia: Mwaka 2024 ulikuwa wa mafanikio