November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ACT kuadhimisha miaka10 ya kuzaliwa kwake mwezi mzima

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

CHAMA cha ACT Wazalendo kinatarajia kuadhimia miaka 10 tangu kuanzishwa kwake kwa kauli mbiu isememayo Miaka 10 ya kupigania maslahi ya wote na Zanzibar yenye mamlaka kamili.

Kauli mbiu hiyo inaakisi inaakisi ahadi ya chama hicho kwa Watanzania ya Taifa la wote, maslahi ya wote na ahadi cha chama hizo kwa Wazanzibari ya Zanzibar mpya, Zanzibar moja, Mamlaka kamili.

Taarifa ya chama hicho kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana imeeleza kwamba maadhimisho ya Miaka 10 ya ACT Wazalendo yatafanyika Mwezi huu hadi Mei 5, 2024.

Kwa mujibu wa chama hicho yatapambwa na shughuli mbalimbali za kisiasa na kijamii katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Baadhi ya shughuli hizo ni kama ifuatavyo;

Kongamano la Vijana Zanzibar ambalo litajadili dhima na Wajibu wa Vijana Katika Kuipigania Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja na Zanzibar Yenye Mamlaka Kamili.

Kongamano hili litafanyika Unguja na kuhudhuriwa na mamia ya Vijana wa Zanzibar Pamoja na Viongozi wa Kitaifa wa Chama na Wadau mbalimbali wa mageuzi nchini.

Kutoa kwa Jamii ambapo pamoja na mambo mengine ya kijamii nchi nzima, Wanachama wa ACT Wazalendo Pamoja na Viongozi wa Kitaifa wataweka kambi Wilayani Rufiji kufanya huduma za kijamii kwa waathirika wa Mafuriko.

Vile vile Vijana na Wanawake wa ACT Wazalendo watakusanya na kutoa Misaada kwa Wananchi wa Rufiji.

Mkutano wa Kidemokrasia Moshi, Kilimanjaro tarehe 27/4/2024 ambapo Wanachama wa ACT Wazalendo Nchi nzima watakutana na Kiongozi wa Chama na kujadiliana naye masuala ya Chama chao. Katika Mkutano huo wa Kidemokrasia Nembo mpya ya Chama na Bendera mpya ya Chama vitazinduliwa Rasmi na Kiongozi wa Chama, Doroth Semu.

Mkutano wa Kidemokrasia ni Kikao cha kikatiba na ni wa wazi kwa Wanachama wote watakaokuwa na uwezo wa kufika Moshi. Chama kitaweka utaratibu mzuri kufanikisha wanachama wanaotaka kuhudhuria Mkutano wa Kidemokrasia wa Mwaka huu. #TwenzetuMoshi.

Pamoja na ushiriki huu wa mikutano na makongamano wanachama wa ACT Wazalendo watashiriki shughuli mbalimbali za kijamii kama vile kuchangia damu katika Benki ya Damu ya Taifa, Kufanya usafi kwenye masoko, Kufanya usafi kwenye hospitali na kuwafariji wagonjwa waliolazwa katika hospitali hizo. Shughuli hizi za kijamii zitafanyika kote Tanzania Bara na Zanzibar.

Aidha, kutakuwa na mkesha wa ACT Wazalendo utakuwa Tarehe 04/05/2024 Makao Makuu ya Chama Jengo la Maalim Seif, Magomeni Dar es Salaam na Ofisi Kuu ya Chama Vuga Zanzibar. Mkesha huu utashuhudia kupandishwa kwa Bendera mpya za Chama.

Chama kinatoa rai kwa wanachama wake wote na viongozi nchi nzima, Mikoa yote Tanzania kushiriki maadhimisho haya ya miaka 10 ya Kuzaliwa kwa Chama chetu kwa kufanya shughuli za kijamii na Kupandisha bendera kwenye ofisi zetu zote.