Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar, Othman Masoud Othman, amehimiza mshikamano miongoni mwa wanachama wa chama hicho ili kuwa na chombo Madhubuti katika kupigania mabadiliko na kupata mamlaka kamili ya Zanzibar kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadae.
Amesema safari hiyo muhimu inahitaji chombo imara chenye nguvu moja ya kuleta mabadiliko ya kweli ya kimaendeleo.
Othman, ameyasema hayo leo kwenye hotuba zake katika ziara ya uimarishaji chama ndani ya mkoa wa Magharibi ‘B’ Unguja kichama, kupitia Majimbo ya Kiembesamaki na Dimani.
“ACT Wazalendo ni chombo sahihi na imara sana na umoja wetu ndio silaha yetu kwani kila atayekuja na dhamira ovu akituona tuko Madhubuti atarudi nyuma” alisisitiza Mh. Othman katika kuendelea kuonesha umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano.
Mhe Othman ambayepia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema ni jukumu la kila kiongozi katika ngazi mbalimbali za kichama kutimiza wajibu wake ili kulifanikisha hilo.
Akiwa katika ziara hiyo Makamu alipata fursa ya kufungua tawi Jipya la ACT Wazalendo la ‘Sarayevo’ lenye wanachama 56 lililopo katika Kijiji cha Sarayevo ndani ya Jimbo la Kiembesamaki na kupongeza msimamo makini wa wanachama wa eneo hilo.
Alisema ili kuongeza umadhubuti wa chama, viongozi wa tawi hilo na mengineyo Zanzibar nzima wanatakiwa waongeze idadi ya wanachama na kuthibitisha kutovunjika moyo kwao kimapambano licha ya madhila wanayoyapata inapokaribia kufanyika uchaguzi mkuu.
Amewataka wana ACT Wazalendo wazishinde kasumba zinazoendana na kuitwa majina mabaya na kusimangwa kwani hiyo itakuwa zaidi pigo kwa wanaopenda kutwaa madaraka ili kukidhi maslahi binafsi.
Aidha amewataka viongozi wa chama hicho kuwasaidia wananchi kuhakikisha wanapata vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi na kutoa taarifa kwa viongozi wakuu endapo kutatokea hitilafu ikiwemo kukataliwa na mamlaka husika. Naye mjumbe wa Kamati kuu ya chama hicho Ndugu Ismail Jussa, ameendelea kuwasisitiza Wananchi wa Zanzibar, kupigania haki zao ndani ya muungano pamoja na kuwataka kuielewa vyema historia ya nchi yao ambayo awali ilikuwa ni kitovu cha biashara ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best