Na Penina Malundo, Timesmajira
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Abdulaaziz Abood ameonesha masikitiko makubwa na kuchukizwa na unyanyasaji unaoendelea kwa wafanya biashara wadogo maarufu kama Wamachinga wanaofanya shughuli zao ndani ya Soko Kuu la Chifu Kingalu Mkoani Morogoro.
Unyanyasaji huo ambao unaofanywa na baadhi ya Viongozi wa Soko hilo kwa kushirikiana na baadhi ya Viongozi wa Manispaa ya Morogoro.
Akikemea tabia hiyo Novemba 12 Mwaka huu wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao, baada ya baadhi yao kumfuata Ofisini kwake na kumweleza juu ya kadhia na Hati iliyotolewa na Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inayowataka wafanyabiashara hao kuondoka ndani ya siku saba.
Abood amesema kuwa kuwasumbua wafanyabiashara hao ni kuwakosesha haki yao ya kimsingi ya kujitafutia riziki halali na ni njia mojawapo ya kuondoa imani ya Chama na Serikali kwa wananchi wake.
“Kimsingi Wafanyabiashara hao waliombwa kutoka Barabarani na kuingia ndani ya Soko hilo ili kuondoa msongamano na kuwafanya wawe katika eneo mtambuka ambalo watu wengi huenda kufanya mahitaji yao ya kimsingi,”amesema na kuongeza
” Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dkt. Samia Suluhu Hassan imepanga na imeanza kutekeleza mpango wa kuwainua vijana kiuchumi kwa kuanza kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana, wamama na watu wenye mahitaji maalum ili makundi hayo yaweze kujiajirina kwa kiasi kikubwa makundi hayo ndiyo yanayojishughulisha na biashara ndogondogo kwenye Soko hilo, kwa hiyo kufanya hivyo ni kuwakosesha Amani na kusababisha taharuki kwa wafanyabiashara hao,”amesema.
Amesema utakapowavuruga wafanyabiashara hao utakuwa umeharibu ajira kwa vijana.” leo tunasema tupunguze baadhi ya vibanda bila kuangalia hawa vijana unawapeleka wapi, Mimi kama Mbunge wenu sikubaliani na hilo nitahoji popote…..
…hatuwezi kuzuia vijana wasijiajiri, walikuwa hawataki watu wafanye biashara hapo walitakiwa kuzuia mapema kabla vibanda havijajengwa,”amesema Abood.*
Naye Kasray Dany Mmoja wa wafanyabiashara wadogo na ni mmojawapo ya wahanga wa Hati hiyo alimuomba Rais Samia kutumia vyombo vyake kuangalia uhalali wa jambo hilo ambalo kimsingi linawaumiza wafanyabiashara hao kwani wanaendesha shughuli hizo kwa kutumia mikopo kutoka katika Mabenki mbalimbali, pia wapo eneo la Soko kwa Mkataba halali wa hadi mwaka 2025 na wanalipa kodi ya vibanda hivyo.
More Stories
GST,BGS zafanya majadiliano namna ya kuanzisha mashirikiano katika tafiti na kujengeana uwezo
Utekelezaji wa Mou Tanzania,Burundi waanza rasmi
Profesa Janabi ampongeza Samia kwa uwekezaji MNH