Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Kuanza kutumika kwa majaribio mfumo wa tiketi mtandao abiria wametakiwa kutoa ushirikiano mkubwa ili kufanikisha zoezi hilo ambalo limeanza tarehe 01 April 2022
Akizungumza kwenye kituo cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Magufuli kilichopo Mbezi luis Jijini Dar es Salaam,Kaimu Katibu Mtendaji wa baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za usafiri ardhini Leo Ngowi amesema baada ya kufika kituoni hapo ikiwa ni siku ya kwanza ya utekelezaji wa zoezi la majaribio la ukataji tiketi kwa njia ya MTANDAO baraza limeshuhudia mwitikio ni mkubwa kwakuwa mabasi mengi wameanza utekelezaji wa agizo hilo na abiria wengi wamehamasika na ukataji tiketi kwa njia ya mtandao.
Ngowi amesema matumizi ya mfumo huo ni rahisi na abiria wameanza kuwa na uelewa juu ya faida za ukataji tiketi kwa njia ya mtandao
“Mfumo huu unamuwezesha abiria hata kama hana simu janja anauwezo kwenda kwa wakala wa basi na kusaidiwa kukata tiketi mtandao lakini pia mtu yeyote mwenye simu janja anaweza kumkatia tiketi mwenzie na kusema mfumo huo ni rafiki kwa mtumiaji”alisema Ngowi.
Aidha ametoa maelekezo jinsi ya kutumia mfumo huo,kwanza mtumiaji anatakiwa kwenda kwenye play store kisha kupakua application inayoitwa tiketi mtandao na baada ya kupakua anapata taarifa ya mabasi yote kwenye kiganja chake na mtumiaji atachagua basi gani anataka kusafiri nalo,na kuanza kuingiza taarifa zake kwenye mfumo kama utakavyomwelekeza,
“Taarifa hizo ni kama vile Tarehe ya kusafiri,kituo cha kuanzia safari,kituo cha kumalizia safari,Namba ya simu,siti ya gari,kisha baada ya hapo atapokea taarifa kwamba ombi lake limekubaliwa baada ya kukubaliwa itakuja hatua ya kufanya malipo na baada ya kufanya malipo ujumbe utatumwa kwenye simu yake ya kiganjani.”
Kaimu Katibu Mtendaji wa Latra ccc amesema baraza limejipanga kikamilifu katika utoaji elimu juu faida ya matumizi ya mfumo wa tiketi mtandao kwa abiria kwa njia mbalimbali kama vile kuwafikia kwenye vituo vya mabasi, kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari,mitandao ya kijamii lengo likiwa kuhakikisha agizo hili linatekelezeka na kufanikiwa kwa asilimia mia moja.
Ikumbukwe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya uchukuzi) Gabriel Migire alitangaza kuanza rasmi kwa mfumo wa majaribio ukataji tiketi kwa njia ya mtandao Tarehe 01 April 2022 na mfumo huo wa majaribio utakwenda kwa muda wa miezi mitatu hadi kufika Tarehe 01 Julai 2022 zoezi la ukataji tiketi kwa njia ya mtandao litakuwa ni lazima.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato