March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Regina atangaza neema sekta ya uvuvi Pasiansi endapo atashinda 

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Mgombea Udiwani Kata ya Pasiansi jimboni Ilemela mkoani Mwanza, kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM), Regina Lubala,ameahidi neema kwa wavuvi wa Mwalo wa Bwiru Ziwani,endapo atashinda katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29,2025.

Akizungumza na Timesmajira Online, Regina,amesema changamoto iliopo katika sekta ya uvuvi katika Kata hiyo,ni kutokuwa na elimu ya ufanyaji shughuli  ya uvuvi kisasa wengi wao wanavua kienyeji.

“Nitakapokuwa Diwani nitajitahidi kutafuta wataalam wa uvuvi kwa ajili ya kuwapatia elimu wavuvi wa eneo hili, ili waweze kufanya uvuvi wa kisasa na wenye tija,”amesema Regina.

Pia amesema,Mwalo wa Bwiru Ziwani mazingira yake siyo rafiki na wakati mwingine wanavua na kupoteza mazao ya uvuvi mengi,hivyo endapo atapata ridhaa katika uchaguzi mkuu atatafuta wataalamu wa uvuvi ambao watawapatia elimu itakayowasaidia kufanya shughuli zao kisasa na kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi kama dagaa,fulu na waweze kupata faida na soko la uhakika.

Pia amesema,atashughulikia kero ya ushuru mkubwa ambayo wavuvi na wachuuzi wadogo wadogo wa mazao ya uvuvi kama dagaa na fulu,katika mwalo huo wamekuwa wakilalamikia.

“Mtakapo nipa ridhaa ya kwenda kuwasemea.Nitasema kule Halmashauri ili tuwe na ushirikishwaji wa kuona kwamba ushuru  ulipwe kwa namna gani,kwa sababu wavuvi wanachodai sasa ni kwamba wanalipa ushuru ambao ni mkubwa na siyo sawa na mapato yao,”amesema Regina.

Sanjari na hayo Regina,amesema ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025,imetekelezwa kwa asilimia 100,na miradi mingi ya kimkakati imefanyika ambapo madarasa yamejengwa na kupunguza utoro.

“Siku ikifika Oktoba 29,mwaka huu wananchi niwaombe mkakipe kura Chama Cha Mapinduzi na zijae mpaka zimwagike na baada ya hapoje mtudai maendeleo,”amesema Regina.