Na Grace Gurisha, TimesMajira,Online Dar
AFISA Habari Msaidizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEM), Dominic Mgaya (37) na mwanafunzi wa Chuo Cha Biashara (CBE), Isaya Massawe (22) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kusambaza maudhui mtandaoni bila leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Washtakiwa hao, wamesomewa mashtaka yao jana mbele ya mahakimu wawili tofauti katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam ambao ni Hakimu Mkazi Mwandamizi, Richard Kabate na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Adolph Ulaya mbele ya Hakimu Kabate alidai kuwa Mgaya anatuhumiwa kutenda kosa hilo katika tarehe tofauti kati ya Oktoba 14, 2017 na Septemba Mosi, 2020 ndani ya jijini Dar es Salaam.
Alidai kuwa mshitakiwa, Mgaya alirusha maudhui hayo kupitia chaneli ya Youtube iitwayo CHADEMA Media Tv bila kuwa na leseni kutoka TCRA.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa huyo alikana kuhusika na tuhuma hizo. Wakili Ulaya alidai upelelezi bado haujakamlika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Hakimu Kabate amesema ili mshtakiwa awe nje kwa dhamana anatakiwa awe na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini bondi ya sh. 500,000 kwa kila mmoja.
Mgaya ametimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana, ambapo kesi itatajwa Oktoba 20, 2020.
Wakati huohuo, Wakili wa Serikali, Ulaya alidai mbele ya Hakimu Ruboroga kuwa Massawe (22), anakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni.
Alidai mshtakiwa (Massawe) anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Februari 4, 2019 na Septemba 16, 2020 maeneo tofauti ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Ilidaiwa mshtakiwa huyo, alichapisha maudhui mtandaoni kupitia Channel ya YouTube yenye jina la Isaya Thomas Massawe, bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Baada ya kusomewa shtaka hilo alikana na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Ruboroga, amesema ili mshtakiwa awe kwa dhamana anatakiwa awe na wadhamini wawili waaminifu watakaosaini bondi ya sh. milioni 3 kwa kila mmoja.
Mshitakiwa huyo aliachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana, kesi itatajwa Oktoba 15, mwaka huu.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea