Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar hatavunja Muungano na Tanganyika, bali atasimamia ipasavyo haki za Zanzibar ndani ya Muungano huo.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mjimbini, Jimbo la Mtambile Wilaya ya Mkoani Pemba. Othman amesema Zanzibar ni mshiriki muhimu katika Muungano, lakini kwa miaka mingi imekuwa ikinyimwa haki zake na kuwafanya Wananchi kubaki maskini wa kutupwa.
Amesema wananchi wa Zanzibar hawana sababu ya kuendelea kuwa maskini wa kutupwa. Taifa hili lina rasilimali nyingi, lakini mfumo mbovu wa Muungano ndiyo unaopelekea umasikini wao.
Othman amesisitiza kuwa Zanzibar ni nchi huru inayostahili kupata haki zake zote za msingi bila kupangiwa na upande wa pili.
Ameongeza kuwa mfumo uliopo umekuwa ukiwadhulumu wananchi na kusababisha maisha yao kudorora.

Katika sera zake, Othman ameahidi kuhakikisha wakulima wa Pemba wanarudishiwa heshima yao kupitia uwezeshaji wa zana bora na mbinu za kisasa za kilimo.
Amesema kwa miaka mingi wananchi wamekuwa wakilima kwa juhudi kubwa, lakini hawana wanalokipata zaidi ya machofu.
Ameeleza kuwa Serikali yake itawapatia zana za kisasa na masoko bora ili kilimo kiwe na tija kwa wakulima.
Aidha, ameahidi kuboresha zao la karafuu ambalo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar.
Amesema serikali yake italiacha zao hilo liwe huru kwa wakulima ili waweze kufaidika moja kwa moja na jasho lao.
Katika hatua nyingine, Mgombea huyo ameahidi kuanzisha Mfuko Maalumu wa Zaka endapo atachaguliwa kuwa Rais.
Amesema mfuko huo utalenga kusaidia maskini wenye hali duni ili wajione ni sehemu muhimu ya jamii na kuondokana na dhana ya kutengwa.
Amesema maskini nao ni sehemu ya jamii na serikali yake itaweka mfumo rasmi wa Zaka, ili misaada hiyo iwafikie walengwa na kuwainua katika maisha yao ya kila siku.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo walionyesha matumaini makubwa na kumpa pongezi Othman kwa sera zake.
Zena Ali, mkazi wa Mtambile, amesema kuwa wamechoka na viongozi wanaopanga bila kujali maslahi ya wananchi na sasa wanamuona Othman ana dira ya kweli ya kutetea Zanzibar.
Salim Juma, mkulima wa karafuu kutoka Pemba, amesema wanaona mwanga mpya na kwamba ikiwa karafuu zitaachwa huru, maisha yao yatabadilika sana, hivyo wana imani kubwa na ACT Wazalendo.
Kwa upande wake, kijana Rashid Suleiman amesema wanataka kiongozi atakayetuwezesha vijana kujiajiri kupitia kilimo na biashara, na kwamba Othman amewaonesha njia hiyo.

More Stories
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10