March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya Tani nne za Dawa za Kulevya zateketezwa Dar

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeteketeza zaidi ya tani nne za dawa za kulevya jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya uhalifu huo unaoathiri jamii.

Jumla ya kilo 4,402.02 za dawa hizo zimeteketezwa katika kiwanda cha saruji cha Twiga kilichopo Wazo, ambapo dawa zilizoharibiwa ni pamoja na kilo 2,168.18 za methamphetamine, kilo 1,064.29 za heroin, gramu 326.95 za cocaine, kilo 515.48 za bangi na kilo 653.74 za mirungi.

Dawa hizo zilihifadhiwa kama vielelezo vya mashauri mbalimbali yaliyokuwa mahakamani, baadhi yakiwa yamekwisha kutolewa hukumu na mengine yakiendelea kusikilizwa. Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, mahakama iliridhia vielelezo hivyo kuteketezwa kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika muonekano wake.

Miongoni mwa kesi zinazohusiana na dawa zilizoteketezwa ni ile ya Najim Abdallah Mohamed, iliyohusisha heroin kilo 882.71 na methamphetamine kilo 2,167.29.

Aidha, hukumu zilizotolewa katika kesi za dawa za kulevya ni pamoja na za wahalifu waliopatikana na hatia akiwemo Hassan Azizi na Salum Shaaban Mpangula waliopata kifungo cha maisha, Hemed Juma Mrisho maarufu kwa jina la Hororo aliyehukumiwa kifungo cha maisha, na Ramadhan Shaban Gumbo aliyepewa kifungo cha miaka 30. Wengine ni Irene Dickson Mseluka aliyehukumiwa miaka mitano na Gema Victor Mmasy aliyepewa kifungo cha miaka mitatu.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa DCEA, Florence Khambi, amesema Mamlaka itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kisheria na kiutendaji ili kulinda taifa dhidi ya madhara ya dawa za kulevya.

Ameongeza kuwa DCEA itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya dawa hizo na kuimarisha ushirikiano na wananchi katika vita hivyo.