Na Martha Fatael, Moshi
Wanawake wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro hususani vijana wenye umri wa kati ya miaka 19 hadi 35, wamekuwa wakitumia njia za uzazi wa mpango bila kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wahudumu wa afya.
Wengi wao hufikia maamuzi hayo kwa kushauriwa na marafiki au kupitia taarifa mitandaoni, hali inayowaweka kwenye hatari ya kupata madhara ya kiafya na kisaikolojia.
Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vya Moshi, akiwemo Mwajuma Msumba na Neema Ismael (siyo majina yao halisi)kutoka Chuo cha Kikuu cha Ushirika Moshi, wanasema hawajawahi kupokea elimu ya uzazi wa mpango vyuoni wala katika vituo vya afya na mara nyingi hutegemea taarifa za mitandaoni au ushauri wa marafiki.
Nao wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mwenge, Amina Juma na Mwanaidi Ally(siyo majina yao halisi),wanaeleza kuwa hawajawahi kufikiwa na wahudumu wa afya na wanatumia zaidi vidonge vya dharura (P2) vya kuzuia mimba licha ya kusikia vina madhara.
Hali kama hiyo inajitokeza pia kwa Leah Mushi na Rena Shirima wakazi wa Moshi, wanasema hawajawahi kufuata huduma za uzazi wa mpango katika zahanati ya karibu kutokana na hofu ya kukutana na wahudumu wanaowafahamu.
Leah anasimulia kuwa baada ya kuomba huduma ya sindano kwenye zahanati moja, alijikuta akipata damu nyingi kwa miezi mitatu mfululizo na kulazimika kuacha kutumia njia hiyo, hali iliyomsababisha kubeba ujauzito mwingine bila kutarajia.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Moshi (DMO), Dkt. Juma Mwombokaleo,anakiri kuwa idara yake haijawahi kufika vyuoni kutoa elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango.
“Kwa kawaida shuleni hatufanyi hizo elimu kutokana na sheria zilivyo wanafunzi hawaruhusiwi kushiriki ngono,lakini kwa vyuoni wale ni watu wazima naomba tulichukue na tutalifanyiakazi,japo chuo cha Ushirika hakipo kwenye mamlaka yangu nitaongea na mwenzangu wa Manispaa kuhusu hilo,”anasema Dkt. Mombokaleo.
Anasema wanaume wako nyuma zaidi katika elimu ya afya ya uzazi huku watumiaji wakubwa wa njia za uzazi wa mpango wakiwa wanawake wenye umri wa miaka 19–35,ambao mara nyingi hujitokeza bila waume zao, wengi wao wakiwa hawajaolewa na pia hawako tayari kutumia mpira wa kiumbe(kondomu).
“Hali ya huduma inaridhisha na tunatoa kwa kufuata taratibu zote za kitabibu na kwa kushirkiana na mashirika yasiyo ya kiserikali ambapo tuna jumla ya vituo 118 kati ya hivyo vikiwemo 65 vya serikali na vilivyobaki vinaendeshwa kwa ushirikiano wa serikali na sekta binafsi,”anasema Dkt Mwombokaleo
Aidha, dhana iliyopo imefanya wanawake kushindwa kufuata huduma katika vituo vya afya karibu nao, badala yake kukimbilia vituo binafsi, hospitali kubwa au kuacha kabisa huduma hizo.
Mtaalamu wa afya mjini Moshi, Dkt. William Shamwenda,anasema watoto waliopo shule wanafungwa na dhana na desturi za kiafrika hivyo wanashindwa kutafuta huduma za afya kwa kuhofia kuoenekana wameanza ngono mapema jambo linalohatarisha afya zao za uzazi.
“Vijana wengi wanakwepa kwenda kupata huduma sahihi za afya kwa kuogopa wataonekanaje hatari yake wanaishia kupata maambukizi ya magonjwa, wanapata mimba zisizotarajiwa na wanaishia kutoa mimba kwa njia zisizosalama.Wanafanya hivyo sababu ya hofu ama uoga wa kuonekana na wahudumu wanaowafahamu,”anasema Dkt. Shamwenda.
Kwa upande wake Mtaalamu wa afya ya uzazi jijini Arusha Dkt. Agnes Mushi,anasisitiza kuwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango bila ushauri wa kitaalamu ni hatari. Baadhi ya dawa zinaweza kuathiri afya ya mfumo wa uzazi, kuongeza hatari ya kutokwa damu nyingi au hata kusababisha upungufu wa damu mwilini.
“Ni lazima huduma hizi zipelekwe moja kwa moja vyuoni na vijijini ili vijana na wanawake wapate elimu sahihi kabla ya kuanza kutumia,”anasema Dkt.Mushi.
Mtaalamu wa sheria, Evarist Ambros,anasema kwa mujibu wa mwongozo na viwango vya kitaifa vya uzazi wa mpango (2013), unatoa maelekezo rasmi kwa utendaji wa huduma za uzazi wa mpango na kiwango kinachotarajiwa cha ubora katika utoaji huduma.
Ambapo uzazi wa mpango ni haki ya binadamu, watu wote wana haki ya kupata taarifa, huduma na vifaa vya kushauri jinsi ya kupanga familia yao na lazima kuwe na elimu kwa jamii kuhusu njia mbalimbali za uzazi wa mpango na ushauri wa kina kabla ya kuchagua njia.
Sera ya Idadi ya Watu ya 2006, serikali iliahidi kuwaelimisha wanawake kuhusu manufaa ya uzazi wa mpango, na Sera ya Taifa ya Afya ya 2007 inasisitiza utoaji wa huduma bure kwa wajawazito na watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango.
Anasema vilevile, Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya IV,umeipa kipaumbele huduma hii ili kuchelewesha umri wa kuzaa kwa mara ya kwanza na kuwapa wanawake ridhaa ya kuamua idadi ya watoto.
Mwanasheria huyo anasema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 11(2), inaitaka serikali kuhakikisha ustawi wa wananchi kwa kutoa huduma bora za afya.
Ilhali Ilani ya CCM 2025–2030 imeweka afya kuwa kiini cha utekelezaji, ikiahidi kuongeza vituo vya afya na kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango.
Hata hivyo, tafiti zinaonesha pengo kubwa kati ya sera na hali halisi. Utafiti wa Chuwa na Christopher (2025) ulibaini kuwa matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango nchini bado ni chini sana, huku hofu ya madhara na ukosefu wa elimu sahihi vikichangia.
Utafiti mwingine katika wilaya ya Tarime (Machinda, Mbonile na Mtae) ulionesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wanaume wanaelewa dhana ya uzazi wa mpango lakini wachache hujihusisha katika maamuzi, hali inayozidisha mzigo kwa wanawake pekee.
Changamoto hii inaibua swali kuhusu utekelezaji wa sheria na sera zilizopo. Wataalamu wanashauri serikali za mitaa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kuongeza programu rafiki kwa vijana na kuhusisha wanaume katika elimu ya afya ya uzazi.
Bila hatua hizo, wanawake wa Moshi na maeneo mengine ya Tanzania wataendelea kukabiliana na madhara ya kutumia njia za uzazi wa mpango bila mwongozo wa kitaalamu.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina