Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online- Mwanza
Wananchi wa Kisiwa cha Bezi, kilichopo Kata ya Kayenze, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili, zikiwemo ukamilishaji wa zahanati, miundombinu ya barabara, huduma ya maji safi na salama pamoja na nishati ya umeme.
Kisiwa hicho chenye wakazi takribani 6,000, ambao shughuli yao kuu ni uvuvi, kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji licha ya kuzungukwa na Ziwa Victori pamoja na changamoto ya barabara na huduma za afya.

Mmoja wa wakazi wa kisiwa hicho akizungumza na Timesmajira online Esther Walioba,amesema kuwa licha ya ujenzi wa zahanati, bado kuna changamoto ya barabara mbovu.
“Wanabezi tunaiomba Serikali itujengee barabara. Zahanati ikianza kufanya kazi, wagonjwa wafikishwe kirahisi. Kwa sasa njia zimejaa mawe, hazipitiki,”amesema Esther na kuongeza:
“Bila miundombinu bora, hata dawa haziwezi kufikishwa kwenye zahanati kwa wakati, hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi,”.
Pendo Waryoba,amesema changamoto nyingine ni upungufu wa nyumba za walimu wanaofundisha katika shule ya msingi Bezi iliopo ndani ya kisiwa hicho pamoja na kuwepo na nishati ya umeme inayotumia jua isiyo ya uhakika inayowanyima watoto kujisomea usiku.
“Umeme unakatika nyakati za usiku, wakati watoto wanajisomea.Hii ni changamoto kubwa kwa maendeleo ya elimu.”
Hassani Nagabona,amesema japo wapo kisiwani na maji yapo lakini siyo salama kwenye kunywa hivyo,ameiomba Serikali na wadau wengine kuweka mazingira ya kupata maji salama kwa ajili ya kunywa na kupikia kwa kuchimba visima au ufanyike utaratibu wa mabomba.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisiwa cha Bezi,James John,amekiri kuwepo kwa changamoto hizo kisiwani humo huku akisisitiza kuwa, barabara kutoka gati la Bezi hadi kwenye zahanati ina urefu wa takribani kilomita moja, lakini ni ya vumbi na mawe mengi, hali inayoweza kuchelewesha utoaji wa huduma kwa wagonjwa au hata kuwasababishia madhara.
“Kumbeba mgonjwa umbali huo kwenye barabara mbovu ni changamoto kubwa. Tunaomba Serikali kupitia TARURA ikamilishe barabara hii ili iweze kurahisishia wananchi kupata huduma kwani inapitia katika taasisi za serikali kama shule, zahanati, mtandao wa TTCL na ofisi za Serikali ya mtaa,”.
John, amesema,ukipatikana umeme wa uhakika utawawezesha wananchi kukuza uchumi kupitia uvuvi na biashara ndogondogo, huku pia ukichochea ulinzi wa kisiwa hicho.Kwani kwa sasa nishati hiyo hupatikanaji wake ni wa kusuasua unaweza kuwepo kwa saa mbili na usiwepo kwa saa saba.

Sanjari na hayo John,amekiri kuwepo na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama,kwa sasa wanategemea maji kutoka nchi kavu Kayenze ambayo usafirishaji kupitia kivuko cha Mv.Ilemela na hulazimika kununua ndoo ya lita 20 kwa shilingi 1,000.
“Kutokana na joto kisiwani hapa mtu mmoja anaweza kunywa maji lita tano kwa siku,na unakuta familia moja ina watoto watano,inaweza kutumia hadi shilingi 3,000 kwa siku kwa ajili ya maji ya kunywa pekee. Serikali ilituahidi maji kufikia Machi mwaka huu, lakini mpaka leo bado hatujaanza kuona huduma hiyo,”.
Hata hivyo ameiomba Serikali kuwapatia boti ya mwendo kasi (speed boat) ambayo itawekwa kwenye gati la Bezi ili kuharakisha usafiri wa wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda hospitali ya Wilaya au Kanda.
“Kuwepo kwa ‘speed boat’,kutasaidia siyo tu kwa wakazi wa Bezi, bali pia wakazi wa visiwa jirani vinavyounda mtaa wa Bezi kupata huduma za afya kutoka katika zahanati ya Bezi pindi itakapokamilika na hata rufaa nje ya kisiwa hicho,” amesema John na kuongeza:
“Wananchi wa Kisiwa cha Bezi wana imani kuwa Serikali yao ni sikivu, hivyo wanaomba ahadi zilizotolewa kuhusu maji, umeme, barabara na ukamilishaji wa zahanati,zitekelezwe kwa wakati ili kuinua ustawi wa maisha yao na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kisiwani hapa,”.
Aidha John, amesema kwa mujibu wa sensa, kisiwa cha Bezi kilikuwa na wakazi 3,602, lakini sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia takribani watu 6,000.
Kisiwa hicho kina jumla ya nyumba 295, huku visiwa vingine viwili vinavyounda mtaa wa Kisiwa cha Bezi ambacho ni Tefu kina nyumba 59 na Nyarubala kina nyumba 22,hivyo kufanya jumla ya nyumba zaidi ya 350.


More Stories
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI