Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya Huduma za Kifedha kwa njia ya simu, Mixx imezindua rasmi Kampeni yake ya ‘Kila Hatua Mixx’, Kanda ya Pwani Kusini kwa lengo la kila Mtanzania anapata huduma za kifedha popote pale alipo.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2010, Mixx ilibeba ndoto ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika huduma za kifedha.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Pwani Kusini , Fadhila Saidi amesema baada ya Miaka 15 ndoto hiyo imekuwa halisi na leo hii Watanzania zaidi ya milioni 20 wanatumia huduma za Mixx kila mwezi huku wakifanya miamala yenye thamani ya takribani shilingi trilioni 6.
Aidha, amesema kupitia mawakala, zaidi ya 200,000 kote nchini, wamewezesha maelfu ya ajira kwa watanzania.
Pia, amesema Wafanyabiashara zaidi ya 500,000 wanapokea malipo salama kidigitali kupitia Mixx.
Vile vile amesema, zaidi ya watanzania milioni 6 wamepata mikopo yenye thamani ya trilioni 1.
Hata hivyo amesema, Watanzania wameweza kuweka zaidi ya bilioni 600 kwenye akiba kupitia huduma zao.

“Hii ni safari ya pamoja na ndio tafsiri sahihi ya Kampeni yetu ya Kila Hatua Mixx.
“Kanda ya Pwani Kusini, hususan mkoa wa Mtwara, ni kitovu cha fursa kedekede ambazo haziwezi kupuuzwa katika kuchochea maendeleo ya nchi yetu,” amesema Fadhila.
Fadhila amesema, Mtwala kuna Kilimo na uvuvi, pia panazalisha korosho bora duniani, na ni lango la biashara ya samaki na mazao ya baharini pamoja na kitovu cha kilimo cha muhogo, mtama na ufuta.
“Tuna gesi asilia na miradi mikubwa ya kimkakati inayochochea ajira na biashara.
“Bandari ya Mtwara: Ni lango la biashara ya kikanda kuelekea Malawi, Msumbiji na Comoro – na nafasi ya kuwa kitovu cha biashara ya kusafirisha mazao na bidhaa za viwandani.

“Fukwe za kipekee, vivutio vya kihistoria na utamaduni wa makabila ya kusini ni hazina kubwa ya utalii ambao unaendelea kukua kwa kasi,” amesema.
Amesema, uzinduzi wa kampeni ya Kila Hatua Mixx mkoani Mtwara si jambo la bahati tu. Ni kutambua kuwa ukuaji wa taifa letu hauwezi kuwa kamili bila Pwani Kusini kuchangia kwa nguvu zake zote.
Hivyo kupitia kampeni hiyo, Yas inaleta huduma zinazogusa maisha ya kila mmoja ambazo ni:
*Bustisha – mkopo wa haraka kukamilisha muamala pale salio linapopungua.

*NivushePlus – mkopo wa papo kwa hapo kusaidia dharura au kuongeza mtaji wa biashara.
*Kibubu – chombo cha kidigitali cha akiba kwa malengo ya baadaye.
*Lipa kwa Simu – suluhisho la malipo salama kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa.
Hata hivyo, huduma hizo zimebuniwa mahsusi kuendana na maisha ya wakazi wa Pwani Kusini, kutoka kwa mkulima wa korosho wa Tandahimba, mvuvi wa Kilwa, mama lishe wa Mtwara mjini, hadi mfanyabiashara anayepeleka bidhaa zake kupitia Bandari ya Mtwara.
Fadhila amesema, Mixx ni zaidi ya huduma ya kifedha, ni rafiki au mshirika wenu wa karibu katika safari na mafanikio yenu ya kifedha.
“Mixx, tunajivunia kuwa huduma ya kifedha pekee nchini iliyotunukiwa cheti cha GSMA ndani ya muda mfupi tu tangu kubadilika kwa chapa.

“Hiki ni kielelezo cha ubora na usalama wa kimataifa na ni dhamana kwamba kila muamala unaoufanya nasi ni salama, thabiti na wa kuaminika.
“Kwa niaba ya Yas na Mixx, ninaahidi kuwa tutaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote wa Pwani Kusini – wakulima, wavuvi, wafanyabiashara, vijana na wanawake kuhakikisha kila mmoja wenu ananufaika na fursa hizi.

More Stories
TAMWA yakumbusha jamii kupinga ukatili wa kijinsia kuelekea siku ta wanawake Duniani
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro