Na Mwandishi wetu,Timesmajira Online
Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud, ameahidi kuikuza kwa kiwango cha juu zaidi sekta ya uvuvi Zanzibar endapo atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi ujao.
Akizungumza na wavuvi wa kijiji cha Shumba, Wilaya ya Micheweni Pemba, Othman alisema Zanzibar ni nchi ya visiwa yenye neema kubwa ya bahari, lakini bado wananchi hawajanufaika ipasavyo na rasilimali hiyo kutokana na kukosekana kwa vyombo vya kisasa vya kuvulia bahari kuu.
Othman amebainisha kuwa Serikali yake itahakikisha wavuvi wa Zanzibar wanapatiwa meli bora na vifaa vya kisasa vya uvuvi badala ya kutegemea boti ndogo na fiber ambazo zimekuwa zikitolewa kwa ubaguzi na bila kuzingatia mahitaji halisi ya wavuvi.
Laiti bahari ya Zanzibar ingetumika ipasavyo, wananchi wote wangenufaika kupitia sekta ya bahari kwa njia moja au nyingine.

Samba na hili Othman amesema Samaki wangekuwa si bidhaa ya anasa bali ya heshima kwa kila familia, na hoteli zetu za kitalii zisingewahi kukosa bidhaa hizo muhimu.
Mgombea huyo ameongeza kuwa Zanzibar inaweza kugeuza sekta ya uvuvi kuwa nguzo kuu ya uchumi sambamba na utalii.
Ametoa mfano wa nchi jirani ya Seychelles ambayo sehemu kubwa ya mapato yake hutokana na uvuvi wa bahari kuu na usafirishaji wa samaki kwenye masoko ya kimataifa. “Kama Seychelles wanaweza, kwa nini sisi tusifanye? .
Amesema Zanzibar ina eneo kubwa la bahari, tuna vijana wengi, na tuna hoteli zinazohitaji samaki kila siku.
Kinachokosekana ni dhamira ya kisiasa na uwekezaji wa kweli,” amesema Othman.
Ameeleza kuwa Serikali yake itajenga vituo maalumu vya baridi na masoko ya kisasa ya samaki Unguja na Pemba ili kuhakikisha wavuvi wanapata bei nzuri ya mazao yao.
Ameeleza kuwa leo hii samaki wanauzwa kwa bei ya chini kwa sababu hakuna uhifadhi, hakuna masoko ya moja kwa moja.
Othman ametaja pia sekta ya uvuvi kama injini ya ajira kwa vijana wa Zanzibar.Alisema ikiwa Serikali itawekeza katika meli za kisasa, viwanda vya kusindika samaki, na masoko ya kimataifa, maelfu ya vijana watapata ajira moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja.
Ametoa mfano wa kijana wa Nungwi, Unguja, anayejulikana kwa jina la Salim, ambaye huendesha boti ndogo ya uvuvi lakini mara nyingi hurudi nyumbani bila mafanikio.
“Ikiwa vijana kama Salim wangekuwa na meli ya kisasa na vifaa vya kufuatilia mikondo ya bahari, leo wangelikuwa wafanyabiashara wakubwa wa samaki badala ya kuishi maisha ya kutegemea,” amesema.
Mbali na meli za kisasa kwa ajili ya uvuvi, Mgombea huyo alisema mkakati huo utaenda sambamba na ununuzi wa boti maalum za uokozi zitakazokuwa zikitumika kusaidia wavuvi wanaopata ajali baharini.
“Haiwezekani kila mwaka tupoteze maisha ya wavuvi kwa sababu hakuna msaada wa haraka. Serikali yangu itanunua boti za uokozi na kuziweka katika maeneo maalum ili pale mvuvi akipata matatizo, awe na uhakika wa msaada wa haraka,” ameeeleza.
Amefafanua kuwa usalama wa wavuvi si suala la hiari bali ni jukumu la Serikali, kwani wavuvi ndio wachangiaji wakubwa wa chakula na mapato ya taifa. “Tukiwalinda wavuvi wetu, tunalinda familia zao na tunalinda uchumi wa Zanzibar,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Othman aliahidi kuhakikisha Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) kinapata vifaa vya kisasa na kufanya kazi zake ipasavyo. Alisema kwa muda mrefu kikosi hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nyenzo bora, jambo lililosababisha bahari ya Zanzibar kuendelea kupoteza rasilimali kupitia magendo.
“KMKM wakipewa meli na vifaa vya kisasa, tutapunguza kwa kiasi kikubwa biashara ya magendo, ambayo imekuwa ikiliangamiza taifa letu. Kwa kufanya hivyo, wavuvi wetu watafanya shughuli zao kwa uhuru na usalama, bila kushindana na wahalifu wanaotumia bahari vibaya,” amesema.
Ameongeza kuwa vyombo vya kisasa vitakavyonunuliwa vitatumikia kazi mbili kwa pamoja: kulinda rasilimali za nchi na kuhakikisha usalama wa wavuvi baharini.
Aidha, Othman aligusia tatizo la ubaguzi katika ugawaji wa vifaa vya uvuvi, akisema Serikali yake itahakikisha kila mvuvi anapata fursa bila kuangalia chama au ukoo wake. “Leo hii tunashuhudia boti za fiber zikigawiwa kwa wachache, huku wengi wakiachwa bila msaada. Serikali yangu haitakuwa ya ubaguzi; itakuwa ya haki na usawa. Vifaa vitatolewa kwa kila mvuvi mwenye sifa bila kujali itikadi yake,” aliongeza.
Katika mkutano huo, wavuvi walipata nafasi ya kueleza changamoto zinazowakabili kila siku.
Mzee Juma Ali, mvuvi mkongwe wa Shumba, amesema: “Tumeishi maisha ya uvuvi kwa vizazi vingi, lakini bado tunatumia boti ndogo zisizo salama. Tunavua karibu na pwani tu kwa sababu hatuna meli za kwenda bahari kuu.
Alisema mara nyingi wanarudi mikono mitupu wakati wanajua samaki wako wingi huko mbali.”amesema.
Amesema wanataka Serikali mpya itakayoona thamani ya wavuvi vijana, watakaowapa fursa ya mikopo nafuu na vifaa bora ili tuende bahari kuu.
Wavuvi wengine walieleza kuwa hata samaki wanaopatikana huuzwa kwa bei ya chini kutokana na ukosefu wa masoko ya uhakika.
“Hoteli zinataka samaki lakini sisi tunashindwa kuwafikia kwa sababu hatuna miundombinu ya baridi ya kuhifadhi samaki.amesema.

More Stories
TAMWA yakumbusha jamii kupinga ukatili wa kijinsia kuelekea siku ta wanawake Duniani
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro