March 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lori lililoharibika lasababisha ajali mbili kwa wakati mmoja

*Wanne wafariki, watano wajeruhiwa.

Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online-Songwe

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limethibitisha kutokea kwa ajali mbili mfululizo zilizopoteza maisha ya watu wanne na kujeruhi watano, baada ya magari mawili kugonga tela la lori lililokuwa limeharibika na kuegeshwa barabarani.

Ajali hizo zilitokea Septemba 29, 2025 majira ya saa 5 usiku eneo la Hanseketwa, Kata ya Ihanda, Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga,amesema ajali ya kwanza ilihusisha gari dogo aina ya Toyota IST lenye namba T.908 CSV, lililokuwa likiendeshwa na Musa Njowela Elton (38), fundi ujenzi mkazi wa Tunduma, ambalo liligonga nyuma ya tela la Lori aina ya Scania lenye namba za usajili T.758 AQP na Tela lake namba T.704 AKH.

Kamnada Senga,amesema katika ajali hiyo, abiria wawili walifariki dunia papo hapo, ambao aliwataja kuwa ni Queen Watson Sampamba (36) na Berdon Mgalla (42), wote wakazi wa Tunduma.

Huku dereva Njowela alinusurika kwa kujeruhiwa vibaya na amelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Mbozi.

Senga ameeleza kuwa dakika chache baadaye, gari jingine aina ya Toyota Surf namba za usajili T.425 EEV, lililokuwa likiendeshwa na Abdul Lugano Mwakapesa (50), nalo liligonga tela hilo hilo.

Ajali hiyo ya pili ilisababisha vifo vya watu wawili ambao ni Emmanuel John Mwangemile (55), mfanyabiashara, na Emmanuel Martin Kandonga (50),Ofisa Elimu Kata ya Mpemba, Halmashauri ya Mji Tunduma,wilayani Momba.

Aidha, watu watano walijeruhiwa katika ajali hizo, ambao ni Winfrida Bakari Mwandule (30),Merisenti John Kimpa (41), Suzie Mwakabonga (28) na Elisha Matata Sindwani (30), pamoja na dereva wa IST,Njowela (38),
wote wakazi wa Mpemba.

Kamanda Senga,amesema ukiacha dereva wa IST ambaye amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbozi, majeruhi wengine wote wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe.

Hata hivyo,amesema dereva wa Toyota Surf, Abdul Mwakapesa, alitoroka mara baada ya ajali na polisi wanaendelea kumsaka ili afikishwe mbele ya sheria.