March 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tindwa aelezea mafanikio makubwa kwenye sekta ya afya

Na Mwandishi wetu

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanzania Health Summit (THS), Dkt. Chakou Tindwa amesema kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 12 ya Mkutano wa afya Tanzania ni ishara ya mchango mkubwa wa Serikali,chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt Tindwa ameyabainaisha hayo mapema leo Octoba 1,2025 katika ufunguzi wa mkutano huo ambao unafanyika jijini Dar es Salaam kwa siku tatu.

Dkt. Tindwa ambaye pia ni mwanzilishi wa THS, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Summit hiyo, kumekuwa na hatua kubwa za maendeleo zilizopatikana kupitia ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na Serikali.

“Tanzania Health Summit inaadhimisha miaka 12 tangu kuanzishwa kwake, na katika kipindi hicho tumeona mafanikio makubwa katika awamu mbalimbali za uongozi, lakini kipindi cha Rais Dkt. Samia kimekuwa cha kipekee kwa ukuaji mkubwa wa idadi ya washiriki na mchango wa Serikali,” amesemaDkt. Tindwa

Dkt. Tindwa , amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani, idadi ya washiriki wa THS ilikuwa wastani wa watu 500 kwa mwaka, lakini hadi sasa imeongezeka hadi kufikia washiriki 1,500 hadi 1,700 kwa kila mkutano.

“Mwaka jana tulifanya Summit Zanzibar na tulikuwa na washiriki zaidi ya 1,600, mwaka huu Dar es Salaam tumefikia zaidi ya washiriki 1,700. Hili ni ongezeko la zaidi ya mara tatu ndani ya kipindi kifupi,” ameongeza

Dkt. Tindwa amesema kuwa mafanikio hayo hayajaja tu katika idadi ya washiriki wa ndani, bali hata kimataifa.

Amesema kabla ya Rais Samia kuingia madarakani, summit ilikuwa inahudhuriwa na washiriki kutoka nchi 15 hadi 20 tu kwa mwaka, lakini kwa sasa idadi hiyo imepanda hadi kufikia washiriki zaidi ya 300 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Mwaka huu tumepokea mabalozi 11 waliokuja kushiriki, jambo linaloonesha wazi kuwa Rais wetu amefungua milango ya ushirikiano wa kimataifa na kuwezesha watu kutoka nje kushiriki mijadala muhimu ya sekta ya afya hapa nchini,” amesema

Aidha, amesema kuwa summit sasa ina uwezo wa kujitegemea kifedha tofauti na zamani ambapo kama mwanzilishi, alilazimika kutumia fedha zake binafsi kuiendesha. Alisema tangu Rais Samia aingie madarakani, hakuna fedha binafsi aliyowahi kutoa kwa ajili ya uendeshaji wa Summit hiyo.

“Makusanyo ya fedha kutoka kwa washiriki yameongezeka mara dufu na Serikali nayo kwa mara ya kwanza imeonyesha dhamira ya dhati kwa kutoa mchango wake kwa kutambua umuhimu wa majadiliano katika kuibua suluhisho kwa changamoto za afya nchini,” amesema

Katika upande wa kitaaluma, Dkt. Tindwa amesema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la machapisho ya kisayansi, kutoka machapisho 10 hadi 15 kwa mwaka hadi kufikia machapisho zaidi ya 200 mwaka huu.

“Machapisho haya ni njia ya wataalamu wa ndani na nje kushirikiana kupitia tafiti na mijadala. Kupitia hayo, miradi mbalimbali ya maendeleo imekuwa ikipatikana na ushirikiano wa kimataifa unaimarishwa,” amesema