March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Exim yawekeza katika uongozi wa wanawake

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaamm

https://www.instagram.com/p/DPN6oTbiGMC/?utm_source=ig_web_copy_link&igsh=MzRlODBiNWFlZA==

BENKI ya Exim Tanzania imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuunga mkono wanawake nchini kwa kudhamini mafunzo ya kipekee ya Mindful Leadership yanayoshirikisha viongozi zaidi ya 150 wa kike kutoka sekta mbalimbali.

Mafunzo hayo, yanayoratibiwa na taasisi ya Mind Matters, yamepangwa kufanyika kwa awamu tatu – Septemba 27, Oktoba 4 na Oktoba 11, 2025 – yakilenga kukuza uongozi wa kina, ustahimilivu, akili ya hisia na ubunifu miongoni mwa wanawake.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Exim Bank, Stanley Kafu, alisema mpango huo ni mwendelezo wa jitihada za benki kupitia Women Empowerment Program (WEP) chini ya mwamvuli wa Exim Cares.

“Tunafurahia kushirikiana na Mind Matters katika kukuza viongozi wanawake. Kupitia WEP, tumekuwa tukitoa mafunzo ya ujasiriamali na mbinu za kuimarisha uwezo wa wanawake, si tu kwa maisha yao binafsi bali pia kwa familia na jamii,” alisema Kafu.

Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Exim, Kauthar D’souza, aliongeza kuwa usawa wa kijinsia ni nguzo kuu ya benki hiyo:

“Tunapoendelea kuwekeza katika wanawake, tunachochea mabadiliko chanya. Hii ni sehemu ya malengo yetu kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa na msaada wa kufanikisha ndoto zao,” alisema.

Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mind Matters, Nadia Ahmed, alisema mafunzo hayo yataleta athari ya moja kwa moja:

“Haya siyo mafunzo ya kawaida. Ni safari ya kubadilisha maisha ya wanawake, kuongeza ustahimilivu wao, na kuimarisha uongozi wa kijamii. Ushirikiano huu na Exim unafanikisha kufikia zaidi ya wanawake 150 moja kwa moja,” alisema.

Mpango wa WEP wa Exim Bank unalenga kufikia wanawake zaidi ya 600,000 ifikapo mwaka 2028, kupitia mafunzo, mitandao ya kibiashara, na mbinu za kuimarisha uongozi wa kihisia na kiuchumi.

Kwa kuchukua jukumu hili, Exim Bank inathibitisha nafasi yake kama benki inayoongoza katika kuunga mkono maendeleo endelevu ya wanawake, sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.