*Ni endapo atachaguliwa kuwa Diwani Pasiansi
*Kukutana na wanawake na kuwapa elimu sahihi ya mikopo na matumizi yake
Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Mgombea Udiwani wa Kata ya Pasiansi, Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Regina Lubala, ameahidi kuwasaidia wanawake wa kata hiyo kunufaika na mikopo ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto zinazowakabili kwa sasa.
Akizungumza na Timesmajira Online,Lubala amesema endapo atapata ridhaa ya kuwa Diwani katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, atahakikisha wanawake wanapewa kipaumbele katika kupata elimu ya mikopo na matumizi sahihi ya fedha hizo.

“Ni yangu ya kugombea nafasi hii ni kuleta maendeleo kwa wananchi wa Pasiansi.Wanawake wengi hawana maendeleo si kwa sababu hawana uwezo bali kukosa elimu ya namna ya kupata mikopo na kutumia fedha hizo kwa ajili ya kuanzisha biashara,”amesema Regina.
Lubala ameeleza kuwa mikopo ya kuwainua wanawake ipo, lakini changamoto ni ukosefu wa uelewa wa jinsi ya kuifikia na kuitumia kwa tija.
Pia amesisitiza kuwa baadhi ya wanawake wamekuwa wakichukua mikopo lakini huishia kuitumia kwa matumizi yasiyo ya maendeleo, jambo linalowaacha katika hali ileile ya umasikini.
“Nitakapochaguliwa kuwa Diwani nitawapa kipaumbele wanawake wa Kata hii,kwanza kwa kukutana nao na kuwapa elimu juu ya upatikanaji wa mikopo,mahali pa kuipata na jinsi ya kuitumia ili iwasaidie kuinua maisha yao na familia zao.Hili ndio nitakalolipa kipaumbele namba moja,”amesema Regina.

Sanjari na hayo,Lubala ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa Kata ya Pasiansi kumpa kura ili aweze kutimiza azma yake ya kuwawezesha wanawake na kuleta maendeleo katika kata hiyo kwa ujumla.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina