Na Mwandisi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
WAKATI Benki ya NMB ikiahidi ushirikiano na mahusiasno mema na wafanyakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke,Mkuu wa Wilaya hiyo (DC), Godwin Gondwe,amesema Program ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), inayotolewa na benki hiyo ni Uwekezaji bora zaidi katika mioyo ya watu.
Hayo yalibainishwa juzi wakati wa Kikao cha Wakuu wa Idara mbalimbali zilizo chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, ambacho kilitumiwa na NMB kutoa elimu juu ya huduma za kibenki zinazotolewa na kuwagusa wafanyakazi hao, sambamba na kuwapa kifungua kinywa.
Akizungumza wakati wa kikao hicho,DC Gondwe amesema amevutiwa na elimu chanya iliyotolewa na NMB na kupongeza huduma rafiki za kibenki, ambapo alienda mbali kwa kuiita CSR, kama uwekezaji bora zaidi katika mioyo ya watu wa makundi mbalimbali, wanaonufaishwa na huduma hiyo.
CSR ni program iliyojikita kutatua changamoto katika Sekta za elimu,afya na majanga kupitia asilimia 1 ya faida yao kila mwaka, na DC Gondwe anaamini kinachofanywa na NMB, ni uwekezaji unaodumu katika mioyo ya wanafunzi wa shule wanazozipa misaada, wazazi, walezi na jamii.
“Ushiriki wa NMB katika matukio ya kijamii ni wa kuigwa tangu nikiwa DC Handeni,Tanga.Niwahakikishie tu kuwa, mnachokifanya ni Uwekezaji Katika Mioyo ya Watu, na ndio uwekezaji bora zaidi. Kazi zenu zinaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli, iliyowekeza katika elimu na afya kwa jamii.
“Ombi langu kwenu,endeleeni kusapoti elimu na afya Temeke, kwani changamoto zitokanazo na maendeleo ni nyingi, ndio maana wanafunzi wanahitaji matuta barabarani, wanahitaji madarasa, madawati na miundombinu mingine, hii ni kutokana na Sera ya Elimu Bure ya Rais Magufuli kuchangamkiwa na wengi,’’ alisema.
Kwa upande wake,Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa NMB, Omary Mtiga, amesema CSR ni program inayotumia asilimia moja ya faida yao kwa mwaka kuhudumia katika sekta hizo, ambako mwaka huu walitenga kiasi cha Sh. Bilioni 1, na kwamba hadi sasa wametumia Sh. Milioni 900 katika kurudisha shukrani kwa jamii.
Aliwataka Wakuu wa Idara katika Manispaa hiyo, kutumia vema elimu waliyopewa na watoa mada mbalimbali walioshiriki kikao hicho, ambako bidhaa mbalimbali za NMB zilinadiwa, zikiwemo Bima ‘BancAssurance,’ Mikopo ya Nyumba ‘NMB Nyanyua Mjengo’ na Huduma za Kidijitali ‘NMB Mkononi.’
Huduma zingine ni mfumo mpya wa Kadi za Malipo Kabla ‘Pre-Payed Card,’ Kadi za Mikopo ‘Credit Card’ Kilimo-Biashara ‘Agri-Business’ na Mikopo Binafsi na Mauzo, mada ambazo zilimkuna DC Gondwe na kuahidi kuwaalika watoa mada hao kufikisha elimu hiyo kwa wafanyakazi wa idara zote za Manispaa hiyo.
Aidha,baada ya kikao hicho, NMB kupitia Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam na Zanzibar, Donatus Richard, ilikabidhi kwa Gondwe msaada wa Viti 20 na meza 20 kwa ajili ya matumizi ya walimu wa Shule ya Msingi Twiga, iliyopo Kata ya Azimio wilayani humo, ili kurahisisha utendaji kazi wa walimu madarasani na ofisini.
Akipokea msaada huo wenye thamani ya Sh.Milioni 5,uliotolewa kupitia CSR, Gondwe aliipongeza NMB kwa kuguswa na mazingira wanayokabiliana nayo walimu na kuamua kutoa msaada huo, aliosema unaenda kurahisisha mazingira ya kufundishia na kukuza ufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo.
“Changamoto katika elimu ni nyingi,na bado zipo.Kama tulivyosikia katika risala hapa, wanahitaji vyumba vya madarasa, madawati na vifaa vya kufundishia viziwi, mashine za ‘photocopy’ na kadhalika, NMB msituchoke. Walimu kwa upande wenu, msaada huu ukawe chachu ya ufundishaji ili kukuza ufaulu,’’ amesema Gondwe.
Mapema akisoma risala kwa niaba ya Mwalimu Mkuu wa Shule, Jackline Amlungi, Mkuu wa Taaluma shuleni hapo,Mary Kajuga, amesema Shule ya Msingi Twiga yenye wanafunzi 1025, inakabiliwa na uhada wa madarasa, vifaa vya Tehama, vifa vya masikio kwa viziwi, ‘photocopy’ na ‘printer’ na walimu wa lugha ya alama.
More Stories
TMDA:Toeni taarifa za ufuatiliaji usalama wa vifaa tiba ,vitendanishi
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo