March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Regina Lubala aahidi  kuboresha barabara Bwiru Ziwani endapo atachaguliwa

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online – Mwanza

Mgombea Udiwani wa Kata ya Pasiansi, Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Regina Lubala, ameahidi kushughulikia kero ya barabara katika Mtaa wa Bwiru Ziwani endapo atachaguliwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na wananchi wa mtaa huo, Septemba 23,2025 wakati wa mkutano wake wa kampeni,Lubala amesema kuwa anatambua changamoto zinazowakabili wakazi wa eneo hilo, hasa suala la miundombinu ya barabara,hivyo atahakikisha linapatiwa suluhisho la kudumu kwa kushirikiana na wananchi endapo atashinda na kuwa Diwani wa Kata hiyo.

“Nashukuru kuona wananchi wameanza kuchukua hatua kwa kupasua miamba na kutengeneza sehemu ya barabara.Hili limenipa chachu zaidi ya kushirikiana nao kwa karibu ili kazi hii iendelee hadi kufikia ziwani, mahali ulipo mwalo wa dagaa,” amesema Lubala.

Huku akisisitiza kuwa ingawa kazi ya kutengeneza barabara ni jukumu la serikali lakini bajeti ya serikali wakati mwingine huwa ndogo, hivyo ushiriki wa wananchi ni muhimu ili maendeleo yaweze kufikiwa kwa haraka.

“Nitahamasisha na kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki katika shughuli za maendeleo, hususani uboreshaji wa miundombinu.Tupo kwenye Jiji la miamba,hivyo tutatumia rasilimali hiyo ya miamba kwa faida yetu katika ujenzi wa miundombinu hasa barabara kwa mtaa huo,”amesema Lubala.

Sanjari na hayo Lubala, amesema  nia na lengo lake la kugombea nafasi ya udiwani ni kuhakikisha maendeleo ya kweli yanawafikia wananchi wa Kata ya Pasiansi, huku akiahidi kuwa kero nyingine zitakazobainishwa na wananchi zitashughulikiwa kwa pamoja kwa ushirikiano.

“Ninaamini kwa kushirikiana tutatatua kero zilizopo na kuijenga Pasiansi mpya yenye maendeleo ya kweli,”amesema Lubala.