March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia awasihi wananchi kuchagua viongozi wenye ushawishi

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

SPIKA wa Bunge na Mgombea Ubunge wa Jimbo jipya la Uyole,Dkt Tulia Ackson, amewataka wananchi kuchagua viongozi wenye ushawishi wa kuwaletea maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, barabara na maji.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 22, 2025, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Itezi, Kata ya Nsalaga, Dkt Tulia amesema maendeleo hayaji kwa bahati bali hutokana na aina ya viongozi wanaochaguliwa.

“Ndugu zangu, shule hazijengwi kwa bahati. Uwepo wa shule ni matokeo ya uongozi tulionao. Hivyo lazima tumchague kiongozi mwenye ushawishi wa kuleta maendeleo,”amesema

Akitolea mfano suala la madawati,Dkt. Tulia amesema changamoto ya wanafunzi wa shule za msingi kukaa chini imemalizika.

“Hakuna mtoto anayekaa chini hapa Uyole. Hata kwenye sekondari, mzigo wa mzazi kubeba dawati kwa mwanafunzi mpya umepunguzwa. Hii ni kazi iliyofanyika chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na mimi,”aliongeza.

Aidha, amesema familia zisizojiweza hupewa sare za shule kila mwaka, huku serikali ikiendelea kuboresha shule kwa kuongeza madarasa na walimu.

Kwa upande wake,Diwani Mteule wa Kata ya Nsalaga kupitia CCM, Clemence Mwandemba, amesema kata hiyo imepata miradi ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 4 ndani ya kipindi cha miaka minne.

“Kwenye sekta ya elimu pekee tumetengewa zaidi ya bilioni 2 na tumepata shule tatu mpya za sekondari, ikiwemo shule ya kisasa ya Nsalaga yenye gharama ya zaidi ya milioni 583,” amesema.

Mmoja wa wananchi wa kata hiyo, Deus Edwin, amesema wananchi wa Jimbo jipya la Uyole wanatarajia maendeleo makubwa zaidi, hususan kwenye afya, elimu, maji na miundombinu.

“Ujio wa Dkt Tulia ni neema tosha kwa wananchi wa Uyole. Tunatarajia uchumi wetu utakua tofauti na ilivyokuwa zamani,”amesema.