March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgodi wa Dhahabu wa Nyanzaga kuanza uzalishaji wa kwanza Januari 2027

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Geita

KAMPUNI ya Uchimbaji Madini ( Sotta Mining Corporation Ltd ) kupitia Mhandisi Mwandamizi wa Mradi, Richard Ojendo, imethibitisha kuwa ujenzi wa mgodi wa dhahabu wa Nyanzaga, unaoendelea katika wilaya ya Sengerema, unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili, ambapo uzalishaji wa kwanza wa dhahabu unatarajiwa kuanza robo ya kwanza ya mwaka 2027.

Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea banda lao katika maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Samia Suluhu Hassan Bombambili mkoani Geita,Ojendo amesema kuwa ujenzi wa mgodi huo unahusisha pia ujenzi wa kinu cha uchenjuaji wa dhahabu, kusaga na kusigina, ambao pia utachukua muda wa miaka miwili. Mradi huu mkubwa umelenga kuinua sekta ya madini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa maeneo jirani.

Kwa mujibu wa Ojendo, tayari nyumba 151 za wananchi waliokuwa wanaishi katika eneo la mradi zimekamilika kujengwa, huku nyumba nyingine 111 zikiwa bado katika hatua za ujenzi.

“Hizi nyumba tunazijenga kwa ajili ya wananchi waliopisha mradi wa mgodi kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.”amesema Ojendo na kuongeza kuwa”tunatarajia nyumba zote zitakamilika ifikapo Oktoba, na hadi sasa utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri,”.

Aidha amesema,kampuni ya Sotta Mining Corporation Ltd inamiliki mgodi huo kwa asilimia 80, huku Serikali ya Tanzania ikimiliki asilimia 20, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa kimkakati kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi moja kwa moja.

Amebainisha kuwa Mradi huu wa Nyanzaga unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya madini nchini, si tu kwa uzalishaji wa dhahabu, bali pia kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya jamii na kukuza uchumi wa Taifa.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Prisca Mapembe, ameishukuru kampuni kwa kuwajali wananchi wa maeneo ya mradi kwa kuwajengea nyumba bora, zenye miundombinu ya msingi kama maji, umeme, na visima vya maji safi.

“Zamani maisha yalikuwa duni, lakini sasa kuna uboreshaji mkubwa. Zaidi ya kujengewa nyumba zenye hadhi, pia tunapewa kipaumbele pale nafasi za ajira za muda mfupi au mrefu zinapotokea,” alisema Prisca kwa furaha.

Naye Felician Bukwimba, ambaye amenufaika kwa kupata ajira kupitia mgodi huo, amesema kuwa uwepo wa mradi huo umekuwa neema kwa wakazi wa eneo hilo, hasa kwa vijana wazawa.

“Ninajivunia kufanya kazi katika mgodi huu. Wazawa tunapewa kipaumbele, hasa kwenye kazi mbalimbali kama utengenezaji wa tofali na shughuli nyingine za ujenzi,” alisema Felician.