April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BoT yapewa Tuzo kwa mchango wake katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini Geita

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online,Geita

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online

BENKI  Kuu ya Tanzania (BoT) imepokea tuzo maalum iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, kama kutambua mchango mkubwa wa taasisi hiyo katika kudhamini na kufanikisha Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.

Tuzo hiyo imekabidhiwa rasmi leo, Septemba 22, 2025, wakati wa uzinduzi wa maonesho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo Bombambili, mkoani Geita, ambapo Waziri Mkuu Majaliwa alihudhuria kama mgeni rasmi.

Kwa niaba ya Benki Kuu ya Tanzania, tuzo hiyo ilipokelewa na Meneja wa Idara ya Mawasiliano wa BoT, Bi. Victoria Msina, ambaye  kwa niaba ya uongozi wa juu wa benki hiyo.

BoT ni moja ya   taasisi muhimu zinazoshiriki maonesho hayo kila mwaka kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya kifedha, pamoja na kutoa huduma mbalimbali zinazolenga kusaidia sekta ya madini, hususan wachimbaji wa madini. 

Maonesho ya Teknolojia ya Madini yamekuwa yakifanyika kwa miaka minane mfululizo, yakilenga kuonyesha maendeleo ya teknolojia katika sekta ya madini, pamoja na kutoa fursa kwa wadau kubadilishana uzoefu, kujenga mahusiano ya kibiashara na kuonesha ubunifu wa kiteknolojia.

Maonyesho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo ” Ukuaji wa Sekta ya Madini ni Matokeo ya Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Uongozi Bora. Shiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba, 2025.” inayolenga kuweka  msisitizo kwa wadau wa sekta ya madini kutumia teknolojia ya kisasa.