Judith Ferdinand
Wasimamizi wa Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS) Mkoa,wametakiwa kuzingatia viwango vya ubora vinafikiwa kama ilivyopangwa kwenye miradi ya dharura ya matengenezo ya barabara (CERC PROJECT),inayoendelea katika Mikoa yao.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara,Mhandisi Rashid Kalimbaga,wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ya wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara(RFB), ya kukagua miradi ya dharura ya matengenezo ya barabara inayofanyika jijini Arusha.

Mhandisi Kalimbaga,amesema sera ya Mfuko wa Barabara ni kuhakikisha miradi yote ya mfuko inafanywa na wakandarasi wazawa hivyo ametoa wito kwa wasimamizi wa TANROADS Mkoa kuhakikisha wakandarasi hao wanafanya kazi kwa weledi na umahiri.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Regnald Massawe,amesema kama mkoa wanatekeleza miradi mitatu ya matengenezo ya barabara ambayo yote ipo kwenye hatua nzuri za utekelezaji.
Mhandisi Massage,amesema Mkoa wa Arusha umepata kiasi cha billion 11, kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu.
“Hapa tupo kwenye mradi wa barabara ya Arusha-Moshi,ambao umeshatekelezwa kwa asilimia 90 na kama unavyoona mkandarasi yupo ‘site’ kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora,”amesema Mhandisi Massawe.

Naye Mhandisi Martin Buchardi, Mkandarasi mzawa kutoka Abemulo Contractors LTD anaefanya mradi wa maboresho ya barabara kuu ya Arusha – Moshi,amesema mradi upo kwenye hatua za mwishoni na wanatarajia kuukamilisha Oktoba mwaka huu kama ilivyopangwa.
Barabara kuu ya Arusha – Namanga na Barabara kuu ya Arusha – Minjingu ni miradi mingine ya dharura ya matengenezo ya barabara inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ufadhili wa Benki ya Dunia mkoani Arusha.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina