March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea Urais wa DP aahidi neema kwa wastafu

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Tabora

CHAMA cha Democratic Party (DP) kimezindua mikutano yake ya kampeni za Urais, Ubunge na udiwani katika uwanja wa stendi ya zamani Mjini Tabora na kuahidi kuboresha mafao ya wastaafu nchini.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika jSeptemba 18,2025 Mjini hapa,ambapo mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha DP, Abdul Juma Mluya amesema akipewa ridhaa kuwa Rais atamaliza kero za wastaafu.

Amebainisha kuwa Serikali itakayoundwa na chama chake itafuta kikokotoo kinachotumika sasa kulipia wastaafu kwa sababu hakiwasaidii bali kinawaongezea presha ya maisha na kusababisha wafe mapema.

‘Falsafa ya DP ni kulinda haki, usawa na maslahi ya wananchi, hivyo kama watapewa ridhaa ya kushika dola Oktoba 29 mwaka huu, ndani ya siku 100 za kwanza atakomesha dhuluma zote kwa wananchi ikiwemo wastaafu,”amesema Mluya.

Mluya ameongeza kuwa serikali ya chama chake itawakopesha nyumba watumishi wote ili wale watakaostaafu wasihangaike bali wawe na mahala pa kuishi na wale watakaoshindwa kulipa mikopo ya nyumba zao watalipa kupitia mafao yao.

“Serikali yetu itawaheshimisha watumishi wote wakiwemo maaskari kwa kuwapa mishahara mizuri ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi mkubwa,”amesema.

Mluya ametaja vipaumbele vingine vilivyoainishwa katika ilani ya uchaguzi ya chama chake kuwa ni kuruhusu uraia pacha kwa diaspora wote ili kuwapa fursa ya kuja kuwekeza nchini, kufumua mikataba ya madini yote na kuanza upya.

Vingine ni kusimamia ipasavyo rasilimali za nchi ili zinufaishe wazawa na kudhibiti utoroshaji malighafi nje ya nchi, pia serikali yake itatunga sheria itakayowabana watoto ili watakapokua wakubwa watunze wazazi wao.

Aidha watadhibiti wanunuzi wanaoibia wakulima, watajenga kiwanda cha asali Tabora, kiwanda cha tumbaku kitahamishwa kutoka Morogoro kuja Tabora, wajawazito watajifungua bure na watapiga marufuku hospitali zote kutoza maiti.

Naye Mgombea Mwenza wa Urais kupitia chama hicho Saadun Abdulrahman Khatibu amesisitiza kuwa chama cha DP kipo kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi hivyo amewaomba wakipigie kura za kutosha ili kishike dola.