Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
KIGODA cha Uprofesa cha Mwalimu Julius Nyerere katika Taaluma za Umajumui wa Afrika kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kimeandaa kongamano kubwa litakalofanyika Septemba 18, 2025, katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ndaki ya Mbeya.
Lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia, vyuo vikuu, washirika wa maendeleo na wananchi ili kujadili kwa kina fursa na changamoto za mwenendo wa uchumi wa Tanzania kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
Mwenyekiti wa Kigoda hicho, Prof. Alexander Makulilo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema kongamano hilo litazungumzia mada kuu kadhaa ikiwemo,
Maudhui na vipaumbele vya Dira ya Taifa 2050.
Misingi ya uchumi jumuishi kwa kuangalia mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2020/21 – 2025/26).Nafasi ya ubia wa sekta binafsi na ya umma katika kukuza maendeleo endelevu nchini.
Prof. Makulilo amebainisha kuwa wazungumzaji watatoka katika taasisi za mipango ya maendeleo, vyuo vikuu, sekta binafsi na watunga sera. Aidha, alieleza kuwa utekelezaji rasmi wa Dira hiyo unatarajiwa kuanza Julai 1, 2026, hivyo maandalizi ya bajeti mpya mwaka huu 2025 ni hatua muhimu ili kuwajengea wananchi na wadau uwezo wa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Prof. Charles Tundui, amesema zaidi ya vijana 36 watashiriki kongamano hilo na watahamasishwa kueneza uelewa kuhusu Dira hiyo miongoni mwa wenzao.
“Katika mitaala yetu tumekuwa tukifundisha Dira ya Taifa iliyopita, lakini sasa tutaweka msisitizo zaidi kwenye Dira mpya ili wanafunzi waelewe vema misingi yake,” amesema .
Naye Mratibu wa Miradi ya Serikali kutoka Tanzania Bara, Msoleni Dakawa, amesema sema Dira ya Taifa 2050 ilipokuwa inatayarishwa wananchi walishirikishwa kwa kiasi kikubwa, hivyo utekelezaji wake lazima uendelee kuhusisha jamii moja kwa moja.
“Walengwa wakuu wa Dira hii ni wananchi na watendaji ngazi zote kuanzia mikoa hadi vijiji. Ikiwa hawataelewa na kushiriki ipasavyo, utekelezaji wake utabaki ndoto,” amesisitiza Dakawa.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi