March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Nchimbi: Tufuate na kuheshimu maamuzi ya chama

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online-Tanga

MGOMBEA mwenza wa kiti cha Urais kupitia Chama Cha Mapindizi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametoa rai kwa wanachama wa CCM kuwa na utaratibu wa kufuata na kuheshimu maamuzi ya chama, hususani katika nafasi za uongozi.

Dkt. Nchimbi ameyasema hayo Septemba 15, mwaka huu, kwenye mkutano na wananchi uliofanyika eneo la Soni, lililopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, akiendelea kukinadi chama hicho ili kiweze kushinda katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29,2025.

Amesema, chama chochote cha siasa kina maamuzi ya kupendekeza yupi ndani ya atapeperusha bendera na kuongeza kuwa kuachwa kuteuliwa katika nafasi ya uongozi haimaanishi kutoteuliwa wakati mwingine.

“Chama kinaamua safari hii aende nani na nani aende wakati mwingine na kuachwa ni kipimo tosha cha kuona mapenzi yako kwa nchi na uaminifu wako kwa chama. Hivyo ni vyema kwa Wana-CCM kuheshimu maamuzi ya chama,”amesema Dkt. Nchimbi.

Aidha Dkt. Nchimbi amewahakikishia wakazi wa Jimbo la Bumbuli Wilaya ya Lushoto kuwa, endapo wataipa ushindi CCM, Serikali chini ya chama hicho itahakikisha inaendelea kuleta maendeleo kwa wakazi wa Jimbo hilo ikiwemo ujenzi wa vituo vitano vya afya, zahanati 6.

Pia kuboresha na kuongeza majengo ya utolewaji huduma ikiwemo jengo la wagonjwa wa mahututi ( ICU) itakayo hudumia wagonjwa hadi 15 kwa siku, katika hospitali ya wilaya hiyo.

Sanjari na kujenga jengo la ‘X-Ray’ na nyumba 20 za wauguzi, pamoja na ukarabati wa miundombinu ya barabara ikiwemo madaraja, vivuko na kuongezwa kwa taa za barabarani.